Korea Kusini. Rafiki mkubwa wa rais wa Korea Kusini, aliyeondolewa madarakani mwaka jana amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ufisadi.
Mshtakiwa Choi Soon-sil ambaye amehukumiwa kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuombea fadhila binti yake, ni wa kwanza katika mlolongo mrefu wa kashfa ya ufisadi iliyosababisha Rais Park Geun Hye kuondolewa mamlakani na kisha kushtakiwa.
Choi ambaye kwa muda mrefu alitumika kama mshauri wa Park, alipatikana na hatia kwa kutumia nafasi yake kushawishi maofisa katika Chuo Kikuu ili binti yake asajiliwe pamoja na kumjazia alama au mitihani ambayo hakuwahi kuifanya.
Mahakama, katika hukumu yake ilisema kwamba Choi “alifanya makosa mengi ambayo yanaonyesha kuwa vitendo vyake vilitokana na upendo wa mama ambaye alitaka mwanawe kufanikiwa,” limeripoti Shirika la Habari la Yonhap.
Maofisa wawili wa zamani katika Chuo Kikuu cha Wanawake cha Ewha kilichopo mjini Seoul pia wamefungwa kwa kushirikiana na Choi.
