Dar es Salaam. Hatima ya dhamana ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu inatarajiwa kujulikana leo, Julai 27 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Uamuzi wa kumpa dhamana au la utatolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Julai 24 jopo la mawakili wanne wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa, Simon Wankyo, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo waliwasilisha hoja mahakamani hapo wakiomba Lissu anyimwe dhamana.
Jopo la mawakili 18 wanaomtetea Lissu, likiongozwa na Fatma Karume na Peter Kibatala liliomba mteja wao apewe dhamana.
Lissu alipelekwa katika Gereza la Segerea na leo hatima ya dhamana yake itajulikana.
Katika shauri linalomkabili, Lissu anadaiwa Julai 17 eneo la Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam alitoa maneno ya uchochezi kuwa, 'Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.'
Anadaiwa kusema vibali vya kazi (working permit) vinatolewa kwa wamishenari wa Kikatoliki tu, huku madhehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji.
Pia, anadaiwa kusema viongozi wakuu wa Serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familia, kabila na ukanda… Acheni woga pazeni sauti… Kila mmoja wetu... Tukawaambie wanaompa msaada wa pesa, Magufuli na Serikali yake kama tulivyowaambia wakati wa Serikali ya makaburu, hii Serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi… yeye ni dikteta uchwara.
Wakili wa Serikali, Kishenyi alidai maneno hayo yalikuwa na lengo la kuleta chuki ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusomewa shtaka, Hakimu Mashauri alimtaka Lissu aeleze kama analikubali shtaka hilo au analikataa.
Lissu alieleza kuwa, “kusema ukweli haijawahi kuwa kosa la jinai kwa hiyo si kweli.”