Dar es Salaam, Novemba 28, 2026.
Tume ya Ushindani (FCC) imeibuka mshindi na kutwaa Tuzo ya Mtoa Huduma Bora wa Umma wa Mwaka (Best Public Service Provider of the Year) katika kipengele cha Kukuza na Kulinda Ushindani wa Haki, Kulinda Maslahi ya Walaji na Kudhibiti Bidhaa Bandia nchini Tanzania.
Tuzo hiyo imepokelewa na Meneja wa Ulinzi wa Walaji wa FCC, Bw. Joshua Msoma, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Bi. Khadija Ngasongwa, katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Ubora za Kitaifa za mwaka 2026, zilizofanyika tarehe 27 Novemba 2026 katika Ukumbi wa Serena Hotel, jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani na Sherehe za Tuzo za Ubora za Kitaifa, zilizoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kuongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb).
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bw. Msoma alisema ushindi huo ni matokeo ya utekelezaji madhubuti wa majukumu ya FCC kwa mujibu wa sheria, sambamba na kuzingatia misingi na tunu kuu za Tume ambazo ni Weledi (Professionalism), Uwazi (Transparency), Kutenda kwa Haki na Bila Upendeleo (Objectivity), Uadilifu (Integrity) na Usiri (Confidentiality).
Alieleza kuwa tuzo hiyo ni kielelezo cha juhudi zinazoendelea kufanywa na FCC katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania linaendeshwa kwa misingi ya ushindani wa haki, walaji wanalindwa dhidi ya vitendo na bidhaa zisizokidhi matakwa ya sheria, na wafanyabiashara wanafuata taratibu zinazowezesha kuwepo kwa mazingira bora ya biashara.
Aidha, mafanikio hayo yanaakisi mchango wa FCC katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia usimamizi wa ushindani wa haki, ambao ni nyenzo muhimu katika kuhamasisha ubunifu, kuongeza ufanisi wa biashara, kulinda maslahi ya walaji na kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa sekta binafsi.
Akihutubia katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, alisisitiza umuhimu wa ubora kama nyenzo ya kimkakati katika kuongeza tija, kuimarisha ushindani, kukuza ubunifu, kulinda walaji na kujenga uchumi endelevu unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Kapinga alieleza kuwa maendeleo endelevu ya viwanda hayawezi kufikiwa bila kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, usalama wa walaji na utekelezaji wa viwango husika. Alibainisha kuwa viwango vinaweka msingi wa pamoja kwa wadau wa viwanda, kurahisisha biashara, kupunguza vikwazo vya kiufundi na kujenga imani kwa walaji.
Katika hotuba yake, Waziri pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa bidhaa ili kulinda walaji na kuhakikisha ushindani wa haki, sambamba na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za Serikali na wadau mbalimbali katika kukuza uchumi wa viwanda.
Kwa upande mwingine, Afisa Uhusiano wa Umma Mkuu wa FCC, Bw. Nsajigwa Wilfred, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume, amewashukuru waandishi wa habari nchini kwa ushirikiano wao wa karibu na Tume katika kuhabarisha Umma kuhusu shughuli, majukumu na taarifa mbalimbali za FCC zenye manufaa kwa walaji na Taifa kwa ujumla.
Bw. Wilfred alisema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masuala ya ushindani wa haki, ulinzi wa walaji na udhibiti wa bidhaa bandia, hivyo kuwezesha Umma kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za kiuchumi na kibiashara.
Aidha, ametoa rai kwa waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na FCC katika kutoa elimu na kuhabarisha Umma kuhusu masuala yanayohusu haki na wajibu wa walaji, mwenendo wa masoko na umuhimu wa kuzingatia sheria za ushindani, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika ustawi wa biashara na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Ushindi huo unaipa FCC chachu ya kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uwazi na uadilifu, huku ikiimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kunakuwepo na mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki, yanayolinda maslahi ya walaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
