Chama cha ACT-Wazalendo Kimejibu Hoja 5 za Bodi ya Korosho

Tarehe 30 Julai 2017, Chama cha ACT Wazalendo kilitoa matokeo ya utafiti wake juu ya usimamizi mbovu wa zoezi la usambazaji wa pembejeo za korosho, hasa pembejeo aina ya Sulphur kwenye mikoa inayozalisha korosho nchini.

Tarehe 2 Agosti 2017, Maafisa Waandamizi wa Bodi ya Korosho, Mwanasheria na Katibu wa Bodi ya Korosho Bi. Ugumba Kilasa na Mkaguzi Mwandamizi wa Ndani wa Bodi ya Korosho Ndugu Christopher Mwaya walifanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kufafanua na kujibu hoja zilizoibuliwa.

Hata hivyo chama cha ACT-Wazalendo kimesema ni dhahiri kuwa Bodi ya Korosho imekwepa kiini cha malalamiko ambayo kimetoa

MAJIBU NA MSIMAMO WA ACT WAZALENDO KUHUSU HOJA ZA BODI YA KOROSHO

Tunapenda kuzijibu hoja zote za Bodi ya Korosho kama ifuatavyo

1. Hoja: Kwamba hakuna pembejeo zenye ubora duni zinazosambazwa na kwenye soko kwa sababu pembejeo zote zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali na TBS.

Jibu: Hoja hii ni nyepesi sana. Bodi ya Korosho inadhani kwamba Sulphur ikishathibitishwa na Mkemia Mkuu na TBS ndio imeshadhibiti tatizo la sulphur zisizo na ubora. Bodi ikumbuke kuwa inayo dhamana kwa kushirikiana na mamlaka za ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sulphur iliyopo kwenye mzunguko ina ubora. Bodi ya Korosho ikumbuke kuwa baada ya kuvunjwa kwa Mfuko wa Wakfu wa Uendelezaji wa Zao la Korosho (CDTIF), yenyewe ndiyo yenye dhamana ya kusimamia ununuzi, usambazaji na ugawaji  wa sulphur yenye viwango. Wakati Maafisa wa Bodi ya Korosho wakitamba mbele ya waandishi wa habari kuwa sulphur yote kwenye mzunguko ina viwango na kwamba tunaosema vinginevyo ni wazushi, jana tarehe 05 Agosti 2017, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara chini ya Mkuu wa Mkoa Nd. Halima Dendego  imekamata tani 20 za sulphur ambazo zimekwisha muda wake wa matumizi.

2. Hoja: Kwamba serikali imenunua sulphur ya kutosha kwa msimu wa mwaka 2017/2018

Jibu: Serikali ilitangaza wazi kwa umma kuwa itasambaza sulphur bure. Huu ndio msingi wa kusimama kwa mfumo wa sulphur ya ruzuku chini ya vyama vya ushirika. Hiki ndicho kiini cha upandaji wa bei wa kasi na uhaba wa sulphur wa kwa sababu waagizaji binafsi walihofia kuingia hasara. Rai yetu kwa mamlaka husika ni kuwa isione soni kukiri udhaifu kuwa haikuwaelimisha vyema wananchi kuwa sulphur ya bure itakuwa pungufu ili nao wajiandae kujinunulia sulphur yao.

3. Hoja: Kwamba serikali imekwishasambaza kwa wakati pembejeo kwa wakulima na iliyobaki bila kusambazwa ni asilimia  29%.

Jibu: Kwenye maeneo mengi pembejeo zimeanza kusambazwa mwezi wa saba. Hata wabunge kutoka vyama mbalimbali waliohojiwa na vyombo vya habari baada ya tamko letu walikiri juu ya uhaba wa sulphur na kuchelewesha kwake. Habari kuwa hadi sasa Bodi inazo hizo asilimia 29 ya pembejeo nayo inasikitisha. Wakati Bodi ikiwa na shehena hiyo, mathalani huko Njengwa, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba Wilaya ya Mtwara vijijini hawajaonja hata kilo moja ya sulphur. Bodi isambaze mapema sana sulphur hiyo badala ya kuendelea kukaa nayo. Wanakaa nayo waifanyie nini?

4. Hoja: Kwamba serikali haiwezi kudhibiti bei ya sulphur.

Jibu: Hii ni hoja dhaifu kuwa serikali haiwezi kupanga bei kwa sababu bei hupangwa na soko lenyewe.  Serikali haioni kuwa inao wajibu wa kuhakikisha kwamba soko haliwanyongi wakulima hasa kwa kupandisha bei kiholela kusikolingana na gharama halisi wanazozitumia kuagiza pembejeo? Serikali inao wajibu wa kuwalinda wakulima. Isikimbie wajibu wake.

5. Hoja: Kwamba wananchi hawajazuiwa kununua sulphur kutoka kwa wafanyabiashara.

Jibu: Bodi imekwepa hoja ya msingi tuliyoitoa. Hakuna aliyesema kuwa wakulima wamezuiwa kununua pembejeo. Tunachosema, kwa kutotoa taarifa sahihi na elimu kwa wakulima na wafanyabiashara, imesababisha uhaba wa sulphur na kupanda kwa bei maradufu. Kusababisha bei kupanda kwa zaidi ya asilimia 100 kwenye maeneo mengi kisha kuwaambia wakulima “ruksa kununua” ni kuwakejeli.
Mpya zaidi Nzee zaidi