Makamu wa Rais: Hatutalisha wilaya itakayokuwa na njaa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha wilaya zao zinazalisha chakula cha kutosha, kwani serikali haitabeba jukumu la kulisha wilaya ambazo zitakumbwa na njaa.

Mama Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia taifa katika sherehe za kilele cha maonyesho ya wakulima 'Nane Nane' yaliyofanyika katika eneo la Ngongo mkoani Lindi, na kusema kuwa serikali itabeba jukumu la kulisha chakula kwa zile wilaya ambazo zitapata maafa ya kiasili na sio kwa uzembe na uvivu.

“Uhakika wa upatakanaji wa chakula unaanza nyumbani kwako, jinsi unavyovuna na kujitengea chakula,tuwaambie wakuu wa wilaya hatutalisha wilaya inayolia njaa kwa uzembe, tutalisha kwa wilaya ambazo zimepata maafa, hivyo niwatake wakuu wa wilaya wahakikishe chakula kinapatikana cha kutosheleza, tukifanya hivyo tutaipunguzia serikali mzigo mkubwa wa kulisha watu”, alisema Mama Samia Suluhu.

Mama Samia aliendelea kwa kuwataka Watanzania kuwa na mshikamano na kufanya uzalishaji kwa kiasi kikubwa, ili nchi ipunguze kuomba misaada.

“Tunaposema Watazania tushikane na tufanye kazi, tunaomba sana, hatuna wajomba wa kutusaidia, naomba sana tushikamane tufanye kazi tuzalishe kwa wingi, tufike pale tunapotaka kwenda”, alisema Mama Samia Suluhu.
Mpya zaidi Nzee zaidi