NGO’s zapewa hadi Aprili 15


SERIKALI imeyakumbusha Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kuwasilisha taarifa za mwaka.

Mashirika hayo yamekumbushwa kufanya hivyo na Msajili kwa mujibu wa Kifungu Na. 29 cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 na Kanuni Na. 10 ya Kanuni za Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2004 (GN 152, 2004) kama ilivyorekebishwa na Kanuni Na. 6 ya Kanuni za Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2014 (GN 8, 2015), kabla ya Aprili mwaka huu.

Kwa mujibu wa Msajili wa NGO’s, S. Katemba, taarifa hiyo ijumuishe taarifa za utendaji kazi, taarifa za fedha zilizokaguliwa, NGO Fomu Na.10 na stakabadhi ya malipo ya ada ya mwaka.

Katemba katika taarifa yake ya jana alisema kuwa mashirika yatakayoshindwa kutekeleza agizo hili ndani ya kipindi tajwa, yatachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.

Mwaka jana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilitangaza kuhakiki Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali kuanzia Agosti 21 hadi 31.

Lengo kuu la zoezi hilo lilikuwa kuhuisha orodha ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, kuboresha kanzi data ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kupima utekelezaji wa majukumu ya Mashirika hayo.

Zoezi hili lilifanyika katika Kanda tano 5. Kanda ya Mashariki ilihudumia mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro. Kanda ya Kati ilihudumia mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma.

Kanda ya Kaskazini ilihudumia mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara. Kanda ya Ziwa ilihudumia mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga wakati kanda ya Nyanda za Juu Kusini ilihudumia mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Katavi, Rukwa, Songwe, Njombe na Iringa.

Wakati wa uhakiki kila shirika linapaswa kuwasilisha cheti halisi cha usajili, nakala ya cheti cha usajili, kujaza fomu ya uhakiki wa NGO, stakabadhi za malipo ya ada ya mwaka tangu kuanzishwa kwa shirika, barua kutoka kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii (Mkoa/Wilaya/Halmashauri/Manispaa) ikithibitisha uwepo wa Ofisi ya Shirika na nakala ya katiba iliyothibitishwa na Msajili wa NGOs.

Mashirika yote ambayo yangeshindwa kuhakikiwa katika vituo yangefutiwa usajili na kuondolewa kwenye orodha ya Msajili wa NGOs.

Taarifa ya Wizara ilieleza kuwa ili kutoa fursa ya kuhuisha kanzi data na benki ya takwimu, usajili wa NGOs ulisitishwa kuanzia Agosti 21 hadi Novemba 30, 2017.

Mpya zaidi Nzee zaidi