Akikosolewa na wengine kutokana na uongozi wake wa kuwa nje ya taifa , rais Paul Biya wa Cameroon hivi karibuni aliitisha mkutano wa baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka miwili.
Uchaguzi wa urais hufanyika mwezi Oktoba na raia wa Cameroon husubiri kusikiza iwapo rais huyo mwenye umri wa miaka 85 atawania muhula mwengine.
Lakini hakuna tangazo kama hilo lililofanywa katika mkutano huo. Bwana Biya amekuwa uongozini tangu 1982, akiwa ni miongoni mwa viongozi wa bara Afrika walioongoza kwa muda mrefu .
Chini ya uongozi wake Cameroon imenusurika mgogoro wa kiuchumi kabla ya kubadilika kutoka kuwa taifa la chama kimoja hadi kuwa na vyama vingi.
Lakini pia taifa hilo limekumbwa na ufisadi wa kiwango cha juu mbali na kuzorota kwa uhuru wa kidemokrasia uliopatikana na kufutiliwa mbali kwa muda wa kipindi cha rais mwaka 2008 ambao ulimruhusu mzee huyo kuwania tena urais mwaka 2011.
