Aliyetumbuliwa amshambulia Trump

Aliyekuwa mkuu wa shirika la upelelezi Marekani FBI James Comey amesema Donald Trump 'hana maadili ya uongozi kushikilia wadhifa wa rais' na ambaye anawachukulia wanawake kama 'kiteweo cha nyama'.

Bwana Comey alikuwa akihojiwa kwa mara ya kwanza kwenye televisheni tangu afutwe kazi na rais Trump mwaka jana.

Ameliambia shirika la habari la ABC kwamba Trump huzusha urongo kila saa na huenda amezuia haki itetendeke.

Saa chache kabla ya mahojiano hayo yapeperushwe, rais Trump alimshambulia Bwana Comey kwa kile anasema ni kusema 'urongo mwingi'.

Comey amekiambia kipindi cha ABC Jumapili usiku: 'Siamini madai yaliopo kumhusu kwamba ana matatizo ya kiakili au katika hatua za kwanza kuugua ugonjwa wa kusahau.'

'Sidhani kwamba ana mapungufu ya kiafya kumuwezesha kuwa rais. Nadhani hana maadili ya kuwa rais'.

"Rais wetu ni lazima aheshimu na afuate maadili ambayo ndio mzizi wa nchi hii. La muhimu zaidi ikiwa ni ukweli. Rais huyu hana uwezo wa kufanya hivyo," Comey amesema.

Baada ya mahojiano kupeperushwa, chama cha Trump - kupitia kamati ya kitaifa ya Republican - kilitoa taarifa ikisema kuwa hatua ya Comey kujitokeza mbele ya umma kunadi kitabu chake imeonyesha kwamba, "utiifu wake wa juu ni kwake mwenyewe".