MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo amesema watu wachache wanaoukosoa waraka wa maaskofu wa kanisa hilo uliotolewa hivi karibuni ni wajinga.
Askofu Dk. Shoo alisema watu wanaopinga waraka huo ni wajinga kwa kuwa unazungumzia mambo ya kweli yanayohusu maisha ya Watanzania wote.
Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu za siku kuu ya Pasaka kwa waumini wa KKKT waliofika kwenye ibada ya kwanza katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini.
“Unajua sisi (maaskofu wa KKKT) tunasikitika sana tunaposema jambo la ukweli, jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote katika ule waraka tulioutoa halafu kuna watu wachache, wajinga mimi nasema; wanasema hawa maaskofu sasa wanasema kwa sababu sadaka zimepungua kanisani," alisema Dk. Shoo.
"Sisi sadaka haijapungua, Wakristo wameendelea kujitoa sana na hawajapungukiwa... Mungu awabariki."
Aidha, askofu huyo licha ya kushukuru waumini wa dhehebu hilo kwa kujitoa kwao na kuwataka kuendelea hivyo, alisisitiza wataendelea kusema ukweli tu na wanaodhani wataharibu ukweli huo waendelee kuuharibu.
Alisema anaamini Watanzania walio wengi, Watanzania wenye hekima, wanaelewa maneno waliyozungumza."Siyo maneno ya kujibu tu haraka haraka, ni maneno ya kututafakarisha."
Katika salamu zake, Askofu Dk. Shoo alisema zaidi:
“Tutaitwa majina mengi, lakini tunajua kiwango cha upotoshaji wa ukweli uliopo katika ule waraka.
"Nasema siyo jambo la hivi hivi, kwa wakati mmoja maaskofu wa makanisa mawili makubwa hapa nchini (ikiwamo Kanisa la Roma) kukaa na kutoa waraka, hatukukaa kusema tupange, tutoe waraka.
“Lakini wapo maaskofu kadhaa wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania wakakaa nao wakaja na ule waraka; Sisi wa KKKT tukakaa tukaja na waraka, ukilinganisha ujumbe ni ule ule, "Sisi tunasema kuna kitu Mungu anataka kutuambia kama Tanzania kupitia ujumbe ule.”
Kutokana na kukosolewa huko kwa waraka, Askofu Shoo alisema anamuomba Mungu awaguse hao ambao wanatumia nguvu nyingi kutaka kupotosha, kutumia nguvu nyingi kupaka matope ili waweze kurejea katika yaliyotajwa humo.
Wakati akianza kutoa salamu hizo, Dk. Shoo alieleza kuwa Pasaka hii wanatoa wito watu waishi maisha ya watu waliowekwa huru, watu waliowekwa hai, watu wenye uhai mpya, wanaothubutu kutoka katika kaburi, kutoka katika "giza lile la dhambi na minyororo inayofunga".
“Tunao wimbo wa 158 (katika kitabu cha Muimbieni Bwana) tunauimba wakati wa mazishi," alisema zaidi."Lakini kwa kweli wimbo ule unasema liko pumziko la mioyo, kwa kweli wimbo ule ni wimbo wa ufufuko, ni wimbo wa kuwaombea wakristo na dunia nzima kututia moyo, kututia matumaini kwamba ndani ya Yesu, huyu aliyefufuka kuna pumziko la milele la mioyo.
"Anasema ninyi mnaosumbuliwa, mnaoelemewa na mizigo, rukeni, kimbieni hima tokeni pangoni mwenu, msienende kwa kuinama.
"Maneno makubwa, maneno yenye uzito… tokeni kwenye pango lenu, kaburi ni alama ya giza, ni alama ya ukombozi inayowaletea watoto wa Mungu uhuru wa kweli ambao ni uhai mpya ulioletwa kwa njia ya kufufuliwa kwa Yesu Kristo.”
Dk. Shoo aliendelea kuhubiri kuwa hofu na mashaka vinaweza vikawafanya watoto wa Mungu wakatamani au wakaendelea kukaa katika giza la kwenye kaburi, kwenye pango lao ambapo kwenye hilo pango, macho yao yameshikwa na yamezoea kuona giza na wanapoambiwa kuna mwanga sasa ambao umetokea kwa Mungu kuondoa lile jiwe kwenye mlango wa kaburi, ule mwanga kwanza unawaumiza macho.
Alisema watu hao pia wanaposikia sauti ya wachache ambao hawataki watoto wa Mungu watoke wakaishi uhai mpya huko nje, basi kwa hofu wanakwenda kubaki katika pango lao.
“Ujumbe wa Pasaka ni huu: Mungu amekwisha kuondoa jiwe, mwanga mpya umetokea, mwanga wa uhai mpya; tutoke katika mapango yetu kwa sababu Yesu ameshinda kifo na mauti, tukatae nguvu zozote zinazopinga uhuru, zinazopinga uhai, zinazoharibu maisha na kufanya wapate hofu," alisema Dk. Shoo.
"Tuwaambie hivi, lile jiwe Mungu amekwishaliondoa, tuwaachie watoto wa Mungu watembee katika mwanga, mwanga wa kweli wa neno la Mungu; kwa sababu ukweli huu hawawezi, hamuwezi kuuficha.”
