Shirika lisilo la kiserikali kutoa Elimu ya TB, tezi dume kwa Vijijini na mashuleni


SHIRIKA lisilo la kiserikali limejiandaa kutoa elimu ya magonjwa ya kifua kikuu, saratani ya matiti na tezi dume kwa wakazi wa vijijini na mashuleni kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Mratibu wa mtandao wa maendeleo ya wanawake, watoto na elimu nchini (INUKA), David Msuya, amesema mafunzo kuhusiana na magonjwa hayo yatafanyika kwenye vijiji vilivyoko kwenye wilaya nane za mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa Msuya, lengo la mafunzo hayo kwa wakazi wa vijijini ni kutokana na ukweli kwamba  jamii inayoishi katika maeneo  hayo ni vigumu kufikiwa na mafunzo, hivyo kuwa na uhitajimkubwa wa kupata elimu hiyo.

Alisema jamii inayoishi vijijini itanufaika na elimu hiyo kwa kujengewa uwezo wa uelewa wa maambukizi ya magonjwa hayo na kuchukua  tahadhari ya kujikinga, hivyo kupunguza ongezeko la kifua kikuu, saratani ya matiti na tezi dume.

“Kuendesha mafunzo hayo kwa jamii za vijijini na wanafunzi wa sekondari tumelenga kuinusuru jamii hiyo ambayo imekuwa na tatizo la elimu ya magonjwa hayo kutokana na kutofikiwa na wataalamu kwa urahisi na kwa wakati,” alisema Msuya.

Hata hivyo, alisema pamoja na serikali kujikita kwenye uhamasishaji wa masuala ya afya kupitia vyombo vya habari, lakini jamii ya vijijini imekuwa vigumu kufikiwa kutokana na mazingira ya ufikaji wa taarifa hizo.

Msuya alizitaja wilaya ambazo zitanufaika na mafunzo ni Handeni, Kilindi, Mkinga na Pangani kwa upande wa Mkoa wa Tanga na nne za Mkoa wa Kilimanjaro.

Aliwaomba wahisani kutoka mashirika na taasisi mbalimbali kusaidia gharama za utoaji wa elimu hiyo  na kwamba  licha ya kuisaidia serikali, lakini pia watakuwa wameinusuru jamii na tatizo la kuathirika kwa magonjwa hayo.

Mpya zaidi Nzee zaidi