Shirikisho la soka nchini Urusi (RFU) lashtakiwa

Shirikisho la soka la Kimataifa FIFA limelishtaki shirikisho la soka nchini Urusi (RFU) ambao ni wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kwa ubaguzi uliofanywa na mashabiki kwenye mechi dhidi ya Ufaransa.

Urusi imeshtakiwa kwenye Kamati ya nidhamu na maadili ya FIFA kutokana na vitendo hviyo ambavyo walifanya mashabiki kwenye mchezo uliopigwa mwezi machi ambao ulikuwa wa kalenda ya FIFA kwa mwezi huo.

Inadaiwa mashabiki waliwazomea kwa kuwaita Nyani wachezaji wa Ufaransa Paul Pogba na Ousmane Dembele, vitendo ambavyo vinapigwa vita michezoni. FIFA imedai ina ushahidi kutoka FARE (Football Against Racism in Europe).

Katika mchezo huo mshambuliaji Kylian Mbappe alifunga mabao mawili, wakati nyota wa Manchester United Pogba pia alifunga bao kwa njia ya adhabu ndogo na kuifanya Ufaransa iondoke na ushindi wa mabao 3-1.

Mchezo huo ulipigwa kwenye uwanja wa Saint Petersburg ambao utatumika kuchezewa nusu fainali ya Kombe la Dunia Julai 10, pamoja na mechi za hatua ya makundi ikiwa kati ya Urusi dhidi ya Misri, Brazil na Costa Rica na Nigeria dhidi ya Argentina.
Mpya zaidi Nzee zaidi