NA REBECA DUWE TANGA
Sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi nchini, huku Mkoa wa Tanga ukiwa na fursa mbalimbali za uwekezaji kutokana na uwepo wa aina tofauti za madini katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza ofisini kwake, Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Tanga, Laurent Bujashi, alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi wanaojihusisha na shughuli za madini ni ukosefu wa mitaji ya kutosha, kutokana na biashara hiyo kuhitaji mtaji mkubwa.
Bujashi alisema wananchi na wadau mbalimbali wanapaswa kufahamu taratibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa katika kufanya shughuli za madini ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Alisema Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini, ambapo aina mbalimbali za madini hupatikana katika maeneo tofauti ya mkoa, isipokuwa madini ya nishati.
“ Aina ya madini zilizopo katika Mkoa wa Tanga ni pamoja na madini ya vito kama rubi na mengine, madini ya metali kama shaba na mengine, madini ya viwandani kama chokaa, pamoja na madini ya ujenzi kama kokoto na mchanga,” alisema Bujashi.
Aliongeza kuwa uwepo wa madini hayo unaifanya Tanga kuwa na fursa kubwa za uwekezaji katika sekta hiyo, hivyo kuwataka wananchi wa ndani na nje ya mkoa, pamoja na wawekezaji kutoka nje ya nchi, kutumia fursa hizo kwa ajili ya kuwekeza na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Bujashi aliwataka wananchi wanaotaka kujihusisha na shughuli za madini kufahamu utaratibu wa kupata leseni.
Alisema mwombaji anatakiwa kuwasilisha taarifa na nyaraka zinazohitajika, ikiwemo namba ya NIDA, barua pepe na taarifa za eneo analokusudia kufanya shughuli za madini.
Alisema baada ya maombi kukamilika, mchakato wa tathmini hufanyika ili kubaini hali ya eneo husika na kama kuna changamoto au athari zinazoweza kujitokeza kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Bujashi pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu aina mbalimbali za leseni za madini kulingana na shughuli wanazokusudia kufanya, zikiwemo leseni za uchimbaji na leseni za utafiti wa madini.
Alisema uelewa wa taratibu hizo utasaidia wananchi kufanya shughuli za madini kwa mujibu wa sheria, kuongeza tija katika sekta hiyo na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, aliwahimiza wananchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi, akieleza kuwa sekta hiyo ina nafasi kubwa katika kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Tanga.

