GOWELE AWABANA MADIWANI TARIME: “SIMAMIENI USAFI, WAANDISHI WACHUNGUZE KATA ZISIZOTEKELEZA”

 


Na Timothy Itembe Tarime.


 Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewataka madiwani kusimamia kwa vitendo usafi wa mazingira katika kata zao, akiwataka pia waandishi wa habari kuibua maeneo yasiyotekeleza zoezi hilo ili kuongeza uwajibikaji na kuifanya Tarime kuwa safi, salama na yenye kuvutia.


Gowele ametoa agizo hilo wakati akihamasisha viongozi na wananchi kushiriki katika usafi wa mazingira, ofisini kwake wakati akiongea na waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa usafi haupaswi kuwa zoezi la msimu au kusubiri maagizo ya viongozi, bali unatakiwa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi.


Amesema usafi wa mazingira ni moja ya nguzo muhimu katika kudhibiti magonjwa ya milipuko, hivyo viongozi katika ngazi za kata wanapaswa kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kulinda usafi wa maeneo yao.


“Nawaomba waandishi wa habari, andikeni habari za usafi wa mazingira. Tembeleeni kila kata na kuandika habari zinazohamasisha usafi wa mazingira. Na kata ambayo haishiriki kufanya usafi wa mazingira, andikeni ili kumwumbua diwani wa eneo husika aone aibu,” alisema Gowele.


Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuufanya usafi kuwa utamaduni wa kudumu, akilinganisha umuhimu wa usafi wa mazingira na mambo mengine ambayo wananchi huyapa kipaumbele katika maisha yao ya kila siku.


“Usafi uwe jadi ya maisha yenu. Mbona mambo mengine mnayapa kipaumbele, kama vile kuvaa nguo safi? Mbona usafi hamuoni kama sehemu ya jadi ya maisha yenu?” alihoji.


AWATAKA MADIWANI KUONGOZA KWA VITENDO

Katika hatua nyingine, Gowele amewasiliana moja kwa moja na baadhi ya madiwani wa kata mbalimbali wilayani Tarime, akiwataka kupanga siku maalumu za kushiriki usafi pamoja na wananchi wao.


Miongoni mwa viongozi aliowasiliana nao ni Diwani wa Kata ya Nyamisangura na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati, ambaye alitakiwa kupanga siku maalumu ya kushiriki usafi katika kata hiyo.


Kwa mujibu wa maelekezo ya Thobias Ghati alisema zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi Ijumaa ya wiki hii, huku viongozi na wananchi wakitakiwa kushirikiana kuhakikisha maeneo mbalimbali ya kata yanakuwa safi na yenye kuvutia.


Gowele pia alijaribu kuwasiliana kwa simu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matele Newland, ili kumtaka kupanga siku maalumu ya usafi katika maeneo yaliyo chini ya halmashauri hiyo. Hata hivyo, juhudi hizo hazikufanikiwa baada ya simu yake kuwa bize.


WAANDISHI WATAKIWA KUIBUA KATA ZISIZOFANYA USAFI.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari na Wapiga Picha Wilayani Tarime, Kalori Jacob, amepongeza juhudi za Mkuu wa Wilaya katika kuhamasisha usafi wa mazingira.


Kalori amesema juhudi hizo zimeanza kuleta mabadiliko katika baadhi ya maeneo kwa kipindi kifupi, akitaja mitaa mbalimbali ya Kata ya Turwa kuwa miongoni mwa maeneo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa safi, yanang'aa na kupitika kwa urahisi.


Amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa usafi, pamoja na kuibua maeneo ambayo hayazingatii usafi ili kuongeza uwajibikaji kwa viongozi na wananchi.


“Usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi. Waandishi wa habari tunapaswa kuendelea kutoa elimu na kuibua maeneo ambayo hayazingatii usafi ili kuongeza uwajibikaji,” alisema.Kalori.


LENGO NI KUDHIBITI MAGONJWA.


Hatua hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuufanya usafi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, sambamba na kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na uchafu wa mazingira.


Wananchi wa Tarime wametakiwa kuhakikisha maeneo ya makazi, biashara, barabara na maeneo ya wazi yanakuwa safi wakati wote, huku viongozi wa mitaa na kata wakisimamia utekelezaji wa zoezi hilo.


Kwa ujumla, ujumbe wa Gowele unaweka msisitizo kwamba “Tarime Safi” inaanzia kwa kila mwananchi, na kwamba usafi unapogeuka kutoka kuwa zoezi la siku moja na kuwa utamaduni wa maisha, jamii hunufaika kwa kuwa na mazingira salama, yenye afya na yanayovutia.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi