Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani watu wanne wakikabiliwa na mashtaka manne ya jinai, likiwemo la kumshambulia askari Polisi, kukaidi amri halali, kumzuia askari Polisi kutekeleza wajibu wake na kuharibu mali kwa makusudi.
Washtakiwa waliopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani hapa ni Goodluck Clement Simbachawene (33), mkazi wa Dar es Salaam, Baraka Rashid Mapunda (34), mkazi wa Mwanza, Steven Henry Makungu (33), mkazi wa Mwanza, pamoja na Willy Onesmo Wandola, mfanyabiashara na mkazi wa Shinyanga, washtakiwa wote wamesomewa mashtaka yao katika Kesi ya Jinai Namba 23860/2026.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Mhe. Stellah Thomas Kiama, Wakili wa Serikali Avance Kaiza, aliieleza mahakama kuwa shtaka la kwanza linawakabili mshtakiwa wa pili Baraka Rashid Mapunda, wa tatu Steven Henry Makungu na wa nne Willy Onesmo Wandola.
Mwendesha mashtaka ameeleza kuwa, mnamo Oktoba 17, 2026, katika eneo la Nyamanoro karibu na Lavena Supermarket, Wilaya ya Ilemela kwa ukaidi na bila halali washtakiwa walimshambulia askari Polisi Issa Ibrahim Issa kwa kumkaba shingoni na kumpiga ngumi ya kifua na hivyo kumsababishia madhara mwilini kinyume na Kifungu cha 241 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Toleo la 2023.
Akiendelea kusoma mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali alieleza kuwa, shtaka la pili linawakabili washtakiwa wote wanne, ambapo inadaiwa kuwa, mnamo Oktoba 17, 2026, katika eneo la Ghana, Wilaya ya Ilemela, kwa pamoja walikaidi amri halali iliyotolewa na Sajenti wa Polisi Jackline, aliyewezeshwa kisheria kutoa amri hiyo.
Washtakiwa hao walikataa kupeleka gari aina ya Range Rover lenye namba za usajili T 189 ANT katika Kituo cha Polisi Kirumba kama walivyoagizwa, kinyume na Kifungu cha 124 cha Kanuni ya adhabu, Sura ya 16 Toleo la 2023.
Kuhusu shtaka la tatu linalowakabili washtakiwa wote la kumzuia afisa wa Polisi kutekeleza wajibu wake, mahakama iliarifiwa kuwa, mnamo Oktoba 17, 2026, katika eneo la Nyamanoro, washtakiwa kwa pamoja walimzuia askari Polisi Issa Ibrahim Issa wakati akitekeleza
