Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, imewakamata raia tisa wa Burundi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Temeke, kufuatia operesheni maalumu ya msako iliyofanyika Oktoba 16, 2026.
Operesheni hiyo imelenga kuimarisha udhibiti wa uingiaji na ukaazi wa raia wa kigeni nchini kwa mujibu wa sheria na taratibu za uhamiaji zinazotumika.
Zoezi hilo la msako lilisimamiwa na Afisa Uhamiaji wa Wilaya ya Temeke, SSI Wilson Ringo, ambaye aliongoza utekelezaji wa operesheni hiyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Wahamiaji hao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kiuhamiaji, yakiwemo kuingia na kukaa nchini kinyume na sheria za uhamiaji. Wataendelea kufanyiwa mahojiano na taratibu nyingine za kisheria zitafuatwa kwa mujibu wa sheria baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Aidha, Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Temeke itaendelea kuimarisha doria na misako katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kudhibiti uingiaji na ukaazi usio halali nchini, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
Wananchi wanahimizwa kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao, ili kusaidia kudhibiti ukiukwaji wa sheria za uhamiaji nchini.
