NA REBECA DUWE TANGA
Mkoa wa Tanga umetajwa kupokea zaidi ya Sh156 bilioni katika uwekezaji wa sekta ya elimu, fedha zinazolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, amesema uwekezaji huo unaofanywa na Serikali ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Dkt. Batilda ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia maandalizi ya maonyesho ya elimu yanayofanyika mkoani Tanga, akisema mkoa huo umejiandaa kikamilifu kwa ajili ya tukio hilo.
Amesema maandalizi hayo yamehusisha pia kuimarisha ulinzi na usalama ili washiriki pamoja na wananchi watakaotembelea maonyesho hayo wawe katika mazingira salama na rafiki.
“Tanga inajivunia kuwa mwenyeji wa maonyesho haya.
Tunawahakikishia Wizara ya Elimu na wananchi kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wote wa maonyesho,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, maonyesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujionea kwa vitendo mchango wa Serikali, taasisi za elimu, watafiti na wabunifu katika kuchochea maendeleo ya Taifa.
Amesema kaulimbiu ya maonyesho hayo, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa 2050,” inaendana na jitihada za Serikali katika kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Dkt. Batilda amesisitiza kuwa kila sekta, taasisi, wizara, mkoa na halmashauri ina wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu Dira hiyo na nafasi yao katika kufanikisha malengo yaliyowekwa.
“Maonyesho haya yataonyesha Tanzania tunayotaka kuifikia ifikapo mwaka 2050. Taasisi za elimu, vyuo vya ufundi, taasisi za utafiti na shule zitaonyesha mchango wao katika kufikia dira hiyo,” amesema.
Aidha alisema zaidi ya washiriki 300 kutoka maeneo mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho hayo, wakiwemo wawakilishi kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya mafunzo na ufundi stadi pamoja na taasisi binafsi zinazohusiana na sayansi na teknolojia.
Dkt. Batilda amesema washiriki hao watapata nafasi ya kuonyesha bunifu, teknolojia na ujuzi mbalimbali unaohusiana na elimu na maendeleo ya Taifa.
Mbali na kuonyesha ubunifu na teknolojia, maonyesho hayo yameelezwa kuwa fursa muhimu kwa vijana wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu.
Vijana hao watapata nafasi ya kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali za elimu ya juu, ikiwemo maelekezo ya namna ya kufanya maombi ya kujiunga na vyuo.
“Vijana wanaoanza mchakato wa kujiunga na vyuo vikuu watapata fursa ya kuelekezwa namna sahihi ya kujaza maombi na kupata taarifa nyingine muhimu kuhusu elimu ya juu,” amesema Dkt. Batilda.
Kwa ujumla, maonyesho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa la kuwakutanisha wadau wa elimu, watafiti, wabunifu na wananchi kwa lengo la kuonyesha namna elimu, ujuzi na ubunifu vinavyoweza kuchangia kufikia malengo ya maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2050.
Mwisho.

