Wachezaji wa Singida United waagwa na Pluijm


BAADA ya kuripotiwa kuwa, Kocha wa Singida United, Hans van Der Pluijm kujiunga na Azam FC, kocha huyo anadaiwa kukaa kikao rasmi na kuwaaga wachezaji wake akiwaambia hatakuwa nao msimu ujao.

Pluijm ameingia makubaliano na Azam kwa ajili ya kuinoa timu hiyo msimu ujao baada ya timu hiyo kuelekea kuachana na Kocha Aristica Cioaba raia wa Romania.

Akizungumza na Championi Jumatano mmoja wa wachezaji wa Singida United ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema, kocha amewaaga rasmi kuwa hatakuwa nao msimu ujao.

“Jana (juzi Jumatatu) usiku tulikutana na Kocha Pluijm tukiwa wachezaji wote, tuliongea masuala mbalimbali lakini pamoja na yote kocha alituaga kuwa msimu ujao hatakuwa na sisi tena hivyo tuendelee kupambana.

“Aliongea mambo mengi lakini tunashukuru kwa kipindi chote ambacho tumekuwa naye amekuwa akitupa hamasa kwa kiasi kikubwa lakini hakuna namna ndiyo hivyo anaondoka tutaendelea kukomaa naamini tutapata kocha mwingine mzuri,” alisema mchezaji huyo.

Pluijm raia wa Uholanzi ndiye kocha wa kwanza kuinoa Singida United tangu ipande ligi kuu msimu huu akisaidiana na Jumanne Chale ingawa aliyepandisha timu alikuwa Fred Felix Minziro.

Meneja wa Singida United, Ibrahim Mohamed akizungumzia ishu ya Pluijm kwenda Azam alisema: “Tunachojua kocha tupo naye na bado ana mkataba na sisi, hizo taarifa za kwenda Azam ndiyo tunazisikia kwako.”