Kikongwe adakwa kwa ujangili wa Twiga


FUNDI ujenzi, Emil Paremen Massawe (80),  mkazi wa Longido, amekamatwa kwa  ujangili akiuza nyama ya Twiga kilo 206, kinyume cha sheria.

Kaimu Ofisa Maliasili Peter Kubingwa, alithibitisha kukamatwa kwa Massawe mkazi wa mtaa wa Buguruni, Namanga, wakati akizungumza na Nipashe juzi.

Alisema mtuhumiwa huyo wa ujangili alikamatwa baada ya ofisi yake kupata taarifa kutoka kwa watu wenye nia njema waliotaja eneo linalotumika kama bucha ya kuuzia nyamapori.

Aliongeza kuwa baada ya upelelezi wao kukamilika alijiridhisha Massawe alikuwa akijishughulisha na uwindaji haramu wa wanyamapori pamoja na kuuza nyama pori.

Alifafanua kuwa ofisi yake ilishirikiana na maofisa wa kikosi maalum cha Kuzuia na Kupambana Ujangili Kanda ya Kaskazini, (KDU).

Kubingwa alisema kutokana thamani ya mnyama huyo, mtuhumiwa akikutwa na hatia atalazimika kulipa faini ya dola 15,000 za Marekani.

Aidha,  alimtaka mwekezaji wa kampuni ya uwindaji Greenmiles kuwa makini katika kudhibiti vitendo vya ujangili kufuatia madai ya kuwa wanyama wengi wanaouawa na majangili hutokea katika kitalu hicho.

Alimtaka kushirikiana na jamii katika kudhibiti uwindaji haramu.

Kwa upande wake, Mkuu wa KDU Kanda ya Kaskazini, Hassan Mnkeni, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa kwa kosa la kujihusisha na ujangili.

Alisema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya kushirikiana na wanasheria wa serikali ilikuweza kuruhusu upelelezi uendelee kwa lengo la kubaini tukio hilo kwa kina zaidi.

Alisema wakati upelelezi huo ukiendelea, mtuhumiwa atakuwa mahabusu.

Mankeni aliwataka wananchi kuwa mabalozi wazuri katika kuwalinda wanyamapori kwani wanyama hao wana haki za kisheria za kuishi na wanatambulika.

Katika hatua nyingine, Mankeni, alitaja maeneo ya Sirkada Namanga kuwa yamekithiri kwa vitendo vya uwindaji haramu na nyamapori zinazopatikana huuzwa mjini Namanga.

Aliwataka wananchi wanaojihusisha na ujangili kuacha vitendo hivyo mara moja kwa sababu Serikali kupitia vyombo vyake itawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.

Mpya zaidi Nzee zaidi