Mwanaume auawa kwa kupondwa kichwa

KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA, EDWARD BUKOMBE.

SIKU chache baada ya mwanamke mmoja kuuawa kinyama kwa kuchinjwa shingo wilayani hapa, tukio lingine la mauaji limefanyika likimhusu kijana Hassan James (25), kuuawa kikatili kwa kupondwa fuvu la kichwa na hatimaye ubongo kutoka nje, huku mwili wake ukikatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea alfajiri usiku wa kuamkia jana katika eneo la Shule ya Msingi Masuguru, Kata ya Masuguru, wilayani Muheza katika barabara kuu ya kutoka Kata ya Kwamkabara, kuelekea Muheza mjini.Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Masuguru wilayani hapa, Shaban Maghembe, alisema alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa wapita njia kuhusu mauaji hayo.Maghembe alisema alipofika katika eneo la tukio alimkuta kijana huyo akiwa amelazwa katikati ya barabara hiyo akiwa ameshafariki dunia, huku fuvu lake likiwa limepondwa na ubongo ukiwa nje.

Aidha, alisema mwili wake ulikutwa ukiwa umekatwa mapanga sehemu za mikono na miguu.Alisema baada ya kuona hali hiyo alipiga simu katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Muheza na askari polisi walifika kuuchukua mwili huo na kuupeleka Hospitali Teule wilayani Muheza.Akielezea matukio ya mauaji wilayani hapo, dereva wa bodaboda, Kiyondo Haidano, alisema vijana wengi wameshikwa na mshtuko mkubwa kutokana na kifo cha kijana mwenzao na mauaji yanayoendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema mpaka sasa chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika huku uchunguzi ukiendelea.Alisema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watuhumiwa waliofanya tukio hilo.

Aidha, Kamanda Bukombe aliwaonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi.
Mpya zaidi Nzee zaidi