WALIMU wa shule za msingi na sekondari Manispaa ya Shinyanga, wameilalamikia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini hapa (Shuwasa), kuzitoza shule bei kubwa za maji sawa na viwanda.
Wamesema wanashangazwa na bei kubwa wakati wanatoa huduma na hawafanyi biashara.
Walisema haiwezekani taasisi hiyo ya serikali kuwekewa bei kubwa ya maji sawa na ya wamiliki wa viwanda, ambapo kuanzia uniti 0 na kuendelea hutozwa Shilingi 2,070.
Wamesema kwamba ilitakiwa wawekewe bei kama za watu binafsi ya unito 0 hadi 5 ambayo hulipiwa Shilingi 1,100. Waliongeza kuwa maji wanayotozwa bei kubwa ni ya matumizi ya shule na walimu.
Walimu walipaza kilio chao hicho wiki iliyopita kwenye kikao cha Baraza la Watumiaji wa Nishati na Maji (Ewura-CCC) mkoani hapa, kilichokuwa na lengo la kutoa elimu kwa walimu hao kufahamu majukumu ya Baraza hilo pamoja na namna ya kuwasilisha kero zao na kutatuliwa.
Mmoja wa walimu hao wakuu, Peter John kutoka Shule ya Msingi Ndala B, alisema taasisi hizo hazipaswi kuwekewa bei kubwa za maji sawa na viwanda, bali zinapaswa kupunguziwa na kutozwa Shilingi 1,100 sawa na watumiaji wa majumbani.
“Tunaiomba Shuwasa kwa kushirikiana na Ewura mtuondolee bei hiyo kubwa ya maji sawa na viwanda, mtuwekee zile za watu binafsi kwani sisi hatufanyi biashara,” alisema John.
Ofisa Uhusiano wa Shuwasa, Nsianel Gerald, alikiri shule hizo kutozwa bei za maji sawa na viwanda, na kubainisha kuwa wao huwa wanaomba viwango hivyo vya bei kupitia Ewura, ambao ndio wanazipitisha baada ya kufanya mchakato wa kuhoji wadau wa maji na kukubaliana nazo.
Kaimu Mwenyekiti wa Ewura-CCC Mkoa wa Shinyanga, Joseph Ndatara, alisema wao kama baraza majukumu yao ni kutetea maslahi ya wananchi, na malalamiko yao huyawasilisha Ewura ili yafanyiwe kazi.
Aidha aliwataka wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wanapotangaziwa kuhudhuria kwenye mchakato wa kupanga bei za maji wawe wanakwenda kwa wingi.
Alisema mara nyingi wengi hawaendi na matokeo yake wachache huzipitisha bei hizo, na zikianza kutumika ndipo wanajitokeza kulalamika kuwa zinawakandamiza.
