Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amegoma kuzindua majengo ya chuo cha Afya cha waganga wasaidizi mkoani Mara kutokana na kutoridhishwa na matumizi ya fedha ya kiasi cha shilingi milion 500 kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi huo.
Hayo yamejiri wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua shughuli za ujenzi na ukarabati wa Majengo ya chuo hicho kilichopo Musoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika kukagua hali ya utoaji huduma za afya mkoani hapo.
“Nimekuja hapa, kazi ya milioni 500 sijaiona kabisa ,kilichofanyika mmepiga rangi, kuta mbovu na siwezi kuwa katika dhambi ya kuhararisha, kwahiyo nimegoma uzinduzi wa majengo haya, na nimeagiza kwa chuo kupata maelezo kwa wote walishiriki na kuahidi kuwachulia hatua wote walishiriki ” amesema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile ametoa onyo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara juu ya fedha nyingine zilizopelekwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo saba vya utoaji wa huduma za Afya katika mkoa wa Mara na kumtaka kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za vituo hivyo ili viweze kuwasaidia wananchi wa Mara.
Mapema mwaka huu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OT-TAMISEMI) kwa kushirikiana ofisi ya Waziri Mkuu, na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ziliagiza kufanyika kwa ukarabati wa vituo vya afya kwenye Mikoa na Halmashauri zote zinazotekeleza miradi ya afya nchini.
