Na Timothy Itembe, Rorya
Mkuu wa Wilaya Rorya mkoani Mara, Simion Chacha amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya, Charles Chacha kuwachukulia hatua kali kiwemo kuwafukuza kazi walimu ambao wanawapachika wanafunzi mimba.
Dc Chacha alimwaagiza Mkurugenzi huyo jana wakati akitoa Hotuba kwa Baraza la Madiwani juu ya msimamo wa serikali kwa wanafunzi ambao wanapata mimba mashuleni kuwa hawana nafasi ya kuendelea na masomo pindi mwanafunzi anapokuwa amegundulika kuwa ana ujauzito kwa hali hiyo kuna haja jamii kuungana na serikali kupiga vita vitendo hivyo ili visiendelee kushamiri.
Mkuu huyo alisema kuwa anatetesi kuwa kuna Mwalimu kutoka Shule ya Msingi Nyamugere pamoja na mwingine wa Shule ya Msingi na Kirogo wanadaiwa kuwapa mimba wanafunzi wao lakini cha kusikitisha walimu hao wapo mitaani wanadunda.
"Mimi nitoe agizo kwako wewe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya ili ukawachukulie hatua walimu hao ambao wanadaiwa kuwapachika mimba wanafunzi wao mashuleni hata kama nikuwafukuza kazi kawafukuze hatutaki kulea watu kama hao na kuwafukuza kazi itakuwa fundisho kwa wengine," alisema Chacha.
Naye Diwani Kata ya Bukwe kupitia Chama Cha Mapinduzi, Charles Wembe alisema kuwa halmashauri hiyo kupitia madiwani wake wanatakiwa kuwa chachu kwa kutoa elimu na kusimamia sheria.
"Watoto wetu wanaharibiwa na baadhi ya walimu ambao sio waaminifu wakiwemo watu wa mitaani kwahali hiyo tunatakiwa kusimamia haki pasipo kuwatetea wahalifu," alisema Wembe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya Charles Chacha alisema kuwa baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaishika serikali miguu ambao mwanafunzi akigundulika kuwa ana ujauzito wanaelewana kinyumbani serikali inakosa ushahidi wakutosha wa kumtia hatiani mtuhumiwa.