Keita achaguliwa kwa mara nyingine kuwa Rais wa Mali


Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita amechaguliwa tena kuwa rais baada ya kushinda kwenye duru ya pili ya uchaguzi na kumshinda mpinzani wake, Soumaila Cisse.

wa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa leo na wizara ya utawala wa ndani, Keita mwenye umri wa miaka 67 amepata asilimia 67.17 ya kura zilizopigwa Jumapili iliyopita, huku mpinzani wake, Cisse akiwa amepata asilimia 32.83. Asilimia 34.5 ya watu ndiyo walijitokeza kupiga kura. Cisse, mwenye umri wa miaka 68 na waziri wa zamani wa fedha pia aligombea urais dhidi ya Keita mwaka 2013.

Chama cha Cisse kimeapa kuyapinga matokeo hayo kwa kutumia njia za kidemokrasia. Siku ya Jumatatu, Cisse alitangaza kwamba atayapinga matokeo na kuwataka wananchi wa Mali kusimama pamoja kupinga udikteta wa udanganyifu, kauli ambayo iliusababisha Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuwepo utulivu.

Keita ni mgombea wa watu
Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, meneja wa kampeni wa Rais Keita, Bacary Treta amesema kamwe hawajawahi kufanya makosa kumsimamisha Keita.

''Katika duru ya kwanza Keita alishinda kwenye mikoa yote ya Mali, nje na ndani ya wilaya ya Bamako. Hivyo mnaweza mkajionea wenyewe kuwa Keita aliwashinda tangu mwanzo wagombea wote. Siku zote tumekuwa tukisema Keita ndiye mgombea wa watu wa Mali,'' alisema Bacary.

Wakati wafuasi wa Keita wakishangilia ushindi, kiongozi wa kampeni wa Cisse, Tiebile Drame ameyapuuza matokeo hayo akisema ni ya uongo. Drame amesema Cisse anapanga kukata rufaa katika Mahakama ya Katiba ili kuyafuta baadhi ya matokeo yaliyo na udanganyifu kwenye mikoa kadhaa.
Mpya zaidi Nzee zaidi