Simba kuiteka Mwanza

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ya Dar es Salaam wakiwa na kikosi kamili walitarajia kutua Mwanza leo asubuhi kwa ajili ya kuivaa Mtibwa Sugar kutoka Manungu, Turiani Morogoro katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini humo.

Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii itakayochezeshwa na refa bora wa msimu uliopita, Elly Sasii atakayesaidiana na Ferdinand Chacha na Hellen Mduma ndiyo itaashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mwaka 2018/19.

Akizungumza na gazeti hili jana,mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Emmanuel Okwi alisema kuwa wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya mchezo huo na msimu mpya wa ligi ambao utaanza kutimua vumbi ifikapo Agosti 22 mwaka huu.

Okwi alisema kuwa wamejiandaa kukutana na ushindani na changamoto kwa kila timu watakayokutana nayo na hilo haliwapi wasiwasi.

"Tuko tayari, tumefanya maandalizi mazuri na ya muda mrefu, tunajua mechi itakuwa na ushindani kwa sababu Mtibwa Sugar ni timu nzuri pia, ila wote tunafahamiana, tunasubiri muda ufike tufanye kazi," alisema mshambuliaji huyo raia wa Uganda.

Naye kiungo Jonas Mkude, amesema wachezaji wa Simba wanajua namna mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanavyotarajia kuona mambo mazuri kutoka kwao.

"Tunajua nini wanachama na mashabiki wetu wanasubiri, tuko tayari kupambana ili kuwapa furaha wanayoisubiri, hakuna kazi rahisi lakini tutajituma ili tusiwaangushe," Mkude alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara alisema kikosi cha mabingwa hao kitatua Mwanza leo asubuhi kwa ajili ya mchezo wao huo dhidi ya mabingwa wa Kombe la FA.

"Timu itakwenda Mwanza kesho (leo) moja kwa moja ikitokea Arusha," alisema Manara.

Aliongeza kuwa anawaomba mashabiki wa timu hiyo waendelee kuiunga mkono timu yao kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa sababu umoja na ushirikiano huleta mafanikio.

Simba itashuka dimbani kuivaa Mtibwa Sugar ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata katika mechi ya kirafiki dhidi ya Arusha United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.