Taasisi ya utafiti wa mifugo kuirejesha Zanzibar katika uasili wake


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ni miongoni mwa mikakati ya kuirejesha Zanzibar katika uasili wake wa kuwa na Taasisi hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kuitembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo iliyopo Langoni, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kujionea hatua za uendelezaji wa majengo ya Taasisi hiyo ambayo ni miongoni mwa Taasisi tatu mpya zilizoanzishwa hivi karibuni katika uongozi wake.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa historia inaonesha kuwa Zanzibar ni ya mwanzo katika Afrika ya Mashariki kuwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ambapo pia uanzishwaji wa Kituo hicho kwa mara nyengine tena ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo lengo lake kuu ni kufanya utafiti wa mifugo kwa kiwango cha juu.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi  na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dk. Kassim Gharib Juma kwa kuanza na hatua nzuri na kueleza matumaini yake makubwa baada ya miaka miwili ya Taasisi hiyo itakavyokuwa.

Aidha, Rais Dk. Shein aliuahidi uongozi wa Taasisi hiyo kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha TZS Bilioni 1.2 zinapatikana katika kuhakikisha Taasisi hiyo inaendelezwa na kuimarika zaidi.

Alieleza kuwa eneo hilo ambalo mwanzo lilikuwa likitumiwa na Kampuni ya ZAPOCO, kwa ajili ya kufuga kuku tayari hivi sasa Serikali imeshamalizana na Kampuni hiyo na limerejeshwa kwa Serikali na uwamuzi uliochukuliwa ni kujengwa Taasisi ya Mifugo ambayo ujenzi wake unandelea.



Mapema Rais Dk. Shein alipata maelezo juu ya ujenzi mpya eneo la Utawala unaoendelea wa Taasisi hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Dk. Kassim Gharib Juma na baadae kutembelea mabanda ambayo yanatayarishwa kwa ajili ya utafiti zikiwemo tafiti kwa ajili ya ngombe, kuku, mbuzi, kondoo, pamoja na mwani.

Pia, Rais Dk. Shein lipata fursa ya kujionea hatua za awali zilizoanza kuchukuliwa na Taasisi hiyo kwa ajili ya utafiti ambapo tayari imeshaanza kupokea wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali duniani wanaofanya tafiti katika eneo hilo na kukutana na mwanafunzi Leanna Kelly kutoka Chuo Kikuu cha California nchini Marekani akishirikiana na wataalamu wazalendo akiwemo Faki Ame Kesi na wengineo.

Nae Dk. Waridi Abdalla Mussa alieleza jinsi hatua za awali wanazozichukua katika kukusanya kuku wa kienyeji kwa ajili ya kuwafanyia utafiti pamoja na kueleza namna ya utafiti wa ngombe wa kienyeji walioufanya na kugundua maradhi ya kichocho na minyoo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba huku akieleza namna ya wanavyokabiliana na maradhi.
Mpya zaidi Nzee zaidi