Wafanyabiashara Dodoma walia na TRA

 Na John Walter-Dodoma

Baadhi ya Wafanyabiashara jijini Dodoma wameilalamikia mamlaka ya mapato [TRA] kwa kuwatoza kodi kwa makadirio na sio kufuata mfumo wa ulipaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wafanyabiashara hao aliejulikana kwa jina la Filimino Munishi alisema  mfumo wa makadirio uliopo hivi sasa si rafiki kwa wafanyabiashara kutokana na hesabu zake kuzidi mauzo ya mwaka jambo ambalo linaathiri mzunguko wa biashara.

‘’Kulipa mapato tunalipa kama kawaida isipokuwa  kuna mfumo ambao  si rafiki sana kwa maana ya kwamba watu wanakufuatilia hata ukiuza kikombe cha mia mbili wanataka utoe risiti na wakati mwingine kodi ambayo tulikuwa tunalipa mwanzo mfano laki tano unapandishiwa mara tatu.”alisema Munishi.

Ameongeza kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kila mfanyabiashara isipokuwa kunahitajika majadiliano ya kina ili kuweza kukusanya mapato zaidi.

Akizungumzia uwepo wa wafanyabiashara wadogo wanaotembeza bidhaa [Machinga] alisema inafanya biashara zao kuwa ngumu kwa sababu wao lazima wauze kwa bei iliyopo na kutoa risiti lakini kwa Machinga wanauza kwa  bei yeyote.

‘’Kinachofanyika ni mfanyabiashara mwenyewe kujiongeza kusema sasa bora nijibadilishe niende mtaani na kuuza kama machinga”alisisitiza

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe alisema kwa sasa Manispaa ya Jiji haijawatambua rasmi wamachinga waliopo katika jiji,hivyo wanashindwa kukusanya ushuru lakini  wameanza kuweka mpango mkakati wa kuwatambua machinga  ili waweze kulipa ushuru.

Aidha wamachinga nao wamedai kuwa manispaa ya jiji inawatambua na pia wanalipa ushuru wa shilingi 1000 kila siku na kupatiwa risiti za karatasi na si kwa kutumia  EFDs Mashine.

‘’Kwa asili ya machinga sio mtu anaefanya biashara katika eneo moja bali ana hama hama na wakati huu ambao bado hatujapanga maeneo yao rasmi lazima changamoto ziwepo,lakini tunafanya mpango wa kuwatambua lakini na wao lazima wajitambue”, alisema Mwamfupe.
Mpya zaidi Nzee zaidi