Chadema yataja sababu za kujitoa kushiriki Uchaguzi


Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema hakiwezi kushiriki chaguzi ndogo za ubunge na udiwani kutokana na namna ambavyo wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya uonevu na Tume ya Uchaguzi nchini NEC.

Akizungumza na wanahabari makao makuu ya Chama hicho leo, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema kamati kuu ya chama chake imekaa na kuona kuwa ni busara kujitoa kwenye uchaguzi huo ili kuepukana na dhuluma ambazo wamekuwa wakifanyiwa na tume hiyo.

" Ukitaka kuamini uchaguzi huu umetawaliwa na dhuluma na uonevu basi angalia namba ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura, fikiria asilimia 85 ya wapiga kura waliojiandikisha hawakujitokeza na hii ni kwa sababu wananchi wenyewe wanaona ni sawa na kupoteza muda kwenda kura.

" Kuna kituo Ukonga kilikuwa na wapiga kura 400 waliojiandikisha lakini waliojitokeza ni 64 tu hii ni aibu, unadhani nani ataenda kupiga kura kama Polisi wanatembea mitaani na magari ya washawasha yenye mabomu na vitambaa vyekundu?," amehoji Mbowe.

Amesema siyo kwamba chama hicho kimejitoa kushiriki kabisa kwenye uchaguzi lakini ni uchaguzi huu mdogo ambao umetangazwa kufanyika mwezi ujao katika baadhi ya kata na jimbo la Liwale.