Mbowe amvaa Makonda, ataka afukuzwe kazi


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe amemvaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kitendo chake cha kusherehekea na Polisi mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya ubunge wa jimbo la Ukonga yaliyompa ushindi mgombea wa CCM, Mwita Waitara.

Mbowe amesema kwa uongozi unaosimamia utawala bora wenye kuzingatia maadili Makonda alipaswa kufukuzwa kazi na siyo kukemewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na kusema kuwa viongozi wa aina hiyo ndiyo huchafua taswira ya majeshi kwa kujihusisha na vyama vya siasa.

Aidha amesema wamepata taarifa za ndani kutoka ndani ya CCM za namna ambavyo Chadema ilivyofanyiwa hujuma huku akisema kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura zaidi ya elfu saba na hata walivyolalamika kwa Tume ya Uchaguzi hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

" Hivi vituo vilitayarishwa ili kuingiza kura za wizi kwa ajili ya CCM kusaidiwa kushinda kwenye uchaguzi, tumeona namna ambavyo vyombo vya serikali  vilivyotajwa na Sheria ya uchaguzi inatamka kutojihusisha na kampeni lakini tunaona mawaziri na wakuu wa mikoa wamekwenda kwenye kampeni na magari ya Serikali na kutoa matamko ya kiserikali bila aibu.

" Tumemuona Waziri Lukuvi, Makonda na wateule wengine wakienda kwenye kampeni na kubadilisha namba magari ya Serikali ili watumie wagombea wa CCM lengo likiwa ni kumfurahisha Rais Magufuli ambaye anataka chama chake kishinde kwa asilimia 100," amesema Mbowe.