" Niko huru na Nchi yangu, Polisi hawana mamlaka ya kuniamulia"


Baada ya kupata matibabu nchini Marekani, staa wa muziki na Mbunge wa Kyadondo Mashariki Uganda, Robert Kyagulanyi 'Bobi Wine' ameweka wazi kuwa ameanza safari yake ya kurudi nyumbani kwao nchini Uganda huku akikataza familia yake kwenda kumpokea.

Bobi Wine ameweka wazi suala hilo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa twitter  mchana wa leo Septemba 19,2018 na kusema kwamba amesikia taarifa kutoka kwa msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, kuwa watairuhusu familia yake pekee kuenda kumpokea katika kiwanja cha ndege ya Entebbe na kudai jambo hilo hatoweza kuliruhusu kwa upande wake kupangiwa watu wa kumpokea.

"Am wondering why these police officers allow themselves to descend so low?, naona wao wanataka kuamua kila kitu kutoka kwangu. Hivyo basi nawaambia hakuna mtu yoyote katika familia yangu ataweza kuja kunipokea kwenye uwanja wa ndege, nitawapata nyumbani kwasababu najua pale walipo", amesema Bobi Wine.

Pamoja na hayo, Bobi Wine ameendelea kwa kusema kuwa "nipo uhuru na nchi yangu, polisi hawana mamlaka ya kuniamulia watu wa kunipokea au mahali ninapotaka kwenda This impunity must stop now. Wama see you friends tomorrow".

Bobi Wine alikuwa nchini Marekani kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa kile kinachodaiwa kimesababishwa na mateso makali aliyoyapata nyakati alipokamatwa na Jeshi la Polisi la Uganda kwa kutuhumiwa kuhusika na kuushambulia msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mdogo eneo la Arua kaskazini mwa nchi ya Uganda.