Na Ferdinand Shayo, Arusha
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelalamikia vitendo vya vitisho kwa wanachama wake na baadhi ya wananchi pamoja na kuondolewa kwa mabango ya mgombea pamoja na bendera za chama hicho katika maeneo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrick Ole Sosopi ambaye pia ni mkuu wa operesheni katika kampeni za chama hicho katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Monduli ,amesema kuwa baadhi ya makada wa CCM wamekua wakiwatishia wananchi na wafanyabiashara kama njia ya kutafuta kuungwa mkono suala ambalo wamelipinga .
Sosopi alisema kuwa kutokana na tathmini waliyoifanya katika kipindi cha kampeni wamebaini kuwa wanaweza kushinda kwa asilimia 75%.
"Tunaipongeza tume ya uchaguzi tayari wamekutana na mawakala wa vyama vyote na kula kiapo mpaka sasa hawajaonesha kuegemea upande wowote" Alisema Sosopi
Aidha ameonya mchezo uliofanyika katika uchaguzi wa jimbo la Kinondoni uliofanyika Februari 16 kwa mawakala wa Chadema kunyimwa hati za kiapo ilihali Mawakala wa CCM walikua na hati hizo
"Tumejipanga kulinda kura na tunawaomba wananchi walinde kura na kuondokana na hofu kuwa hata tukishinda hatutangazwa jambo ambalo halitatokea" Alisema Sosopi
Pia ameitaka tume ya uchaguzi kutoa orodha ya majina ya wasimamizi wa uchaguzi ili waweze kuyafahamu mapema na iwapo wana wasiwasi waweze kutoa taarifa mapema.
Mgombea wa Chama hicho Yonas Masiaya amesema kuwa tayari amejiandaa kwa ushindi licha ya vitisho hivyo wananchi watumie vizuri haki yao ya kupiga kura ili wampate kiongozi wanaemtaka.
