Chama cha Mapinduzi kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kimesema hakuna hata chama kimoja cha upinzani chenye itikadi yake huku pia kikikanusha kurudi ndani ya chama hicho kwa aliyekuwa mwanachama wake na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Lowassa ambaye aliachana na CCM mwaka 2015 baada ya jina lake kukatwa kwenye kinyang'anyiro cha Urais na kujiunga na Chadema amekuwa akitajwa kurejea CCM lakini sasa Polepole amekanusha akisema jambo hilo haliwezekani.
" Hawezi kujiunga yule aah hawezi kwanza yupo Monduli huko akiugulia maumivu ya kushindwa kwenye uchaguzi kwa mgombea wa chama chake.
" Kuhusu itikadi za vyama hakuna mpinzani mwenye nayo, nikiuliza itikadi ya Chadema mnaijua? ya CUF je? ya ACT mnaijua zaidi ukivitaja hivyo vyama unaona mtu mmoja mmoja hawana taasisi," amesema Polepole.
Polepole ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na matokeo ya uchaguzi mdogo uliomalizika ambapo amesema CCM itaendelea kushinda kwenye kila chaguzi kutokana na namna ambavyo wamejitoa kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
