Ferdinand Shayo, Arusha
Katika muendelezo wa operesheni ya ukusanyaji wa mapato , Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk Maulid Suleiman Madeni leo Tarehe 17 Septemba 2018 amefungia zaidi ya vibanda 90 vya wafanyabishara wa stendi ndogo Jijini Arusha kwa kuwa na malimbikizo ya madeni na kukwepa ushuru wa vibanda hivyo pamoja na kutokuwa na leseni za biashara .
Miongoni mwa vibanda vilivyofungiwa ni pamoja na vibanda 69 vinavyomilikiwa na mfanyabiashara maarufu kwa jina la Mouris Makoi anayedaiwa ushuru wa shilingi milioni 85.
Dk Madeni amesema kuwa Makoi ni mdaiwa sugu kwani amekuwa akikwepa kulipa kodi ya serikali kwa muda mefu kitendo kinachopelekea kuinyima mapato Halmashauri na ameagiza alipe deni lote ama ajisalimishe ofisini kwake kabla hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake.
Pia Dk Madeni amesikitishwa na baadhi wafanyabiashara wanaojificha chini ya miamvuli ya vyama vya siasa ili kukwepa kulipa kodi ya serikali na kuwaasa wawe mfano bora katika kuhamasisha zoezi la ulipaji kodi.