Na.Ahmad Mmow, Lindi
WILAYA ya Nachingwea mkoa wa Lindi, jana ilizindua ununuzi wa korosho msimu wa mwaka 2018/2019 ambapo mnada wa kwanza unatarajiwa kufanyika tarehe 24, mwezi huu katika mamlaka ya mji mdogo wa Nachingwea.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Mnero Ngongo, Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango aliwahakikishia wakulima wa zao hilo kwamba serikali imejipanga vema kuhakikisha hakutakuwa na ubabaishaji katika malipo.
Alisema miongoni mwa sababu zinazosababisha malalamiko ni walanguzi kupata upenyo wa kuwadhulumu wakulima na ucheleweshaji wa malipo ya wakulima huku sababu za ucheleweshaji huo zikiwa hazina mashiko bali uzembe unaofanywa kwa makusudi ili kukidhi maslahi binafsi ya wachache.
Aliwaonya watendaji na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) wasiwe sehemu ya watakaochangia kuchelewesha malipo.
"Kuweni waadilifu, ndio sababu mmeapishwa leo. Hatutasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaokiuka kiapo. Hatupo tayari kuona wachache kwa tamaa zao wanasababisha migogoro katika jamii. Atayethubutu kuchezea pesa za wakulima ajue anajitafutia balaa,"alionya Muwango.
