Sakata la Mwandishi aliyeuawa lachukua sura mpya, Marekani yatoa onyo


Rais wa Marekani Donald Trump amekiri huenda mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Kashoggi amefariki na kutishia kuchukuwa hatua kali iwapo itathibitika viongozi wa Saudi Arabia walihusika na kifo chake.

Onyo la Rais huyo wa Marekani limekuja wakati serikali yake ikizidisha ukali juu ya kupotea kwa Khashoggi kulikoibua ghadhabu ya Kimataifa. Trump amesema kwa sasa wanasubiri majibu ya uchunguzi kabla ya kutoa taarifa ya aina yoyote.

Kabla ya Trump kuzungumza siku ya Alhamisi utawala wake ulitangaza kuwa waziri wake wa fedha Steven Mnuchin amejiondoa kwenye mkutano mkubwa wa uwekezaji unaoandaliwa na Saudi Arabia.

Wakati huo huo maafisa wa Marekani wakisema kuwa Waziri wa mambo ya kigeni Mike Pompeo alimuonya mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuwa uaminifu wake kama kiongozi wa siku za usoni wa taifa hilo uko mashakani.

Pompeo amesema Saudi Arabia inapaswa ipewe muda wa siku chache zijazo wa kufanya uchunguzi wa wazi na unaoaminika kabla Marekani haijaamua namna itakavyojibu.

Tamko la Rais wa Marekani Donald Trump linatoa ishara ya haja ya kuongeza kasi katika uchunguzi juu ya kupotea kwa mwanahabari Jamal Kashoggi.

Kashoggi alieonekana mara ya mwisho tarehe 2 Oktoba alipokuwa akiingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, nchini Uturuki. Kashoggi alikuwa mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme Muhammed Bin Salman.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items