Umoja wa Ulaya (EU) umeahidi kuimarisha misaada yake kwenye sekta ya kilimo nchini kwa kuongeza kiwango cha ufadhili kwenye miradi mbalimbali ya sekta hiyo inayoitekeleza kwa kushirikiana na serikali na wadau wa kilimo.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Balozi wa Umoja huo nchini, Charles Stuart wakati akihutubia kwenye Maonesho ya Soko la Wakulima yaliyofanyika juzi chini ya ufadhili wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kuhudhuriwa na wadau kadhaa wa masuala ya chakula.
Balozi, Stuart alisema kuwa umoja huo unavutiwa na namna ambavyo serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo kwa kushirikiana na wadau ukiwamo umoja huo. Alisema:
Serikali ya Tanzania ni moja kati ya wadau wakubwa na muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha barani Afrika hasa kwa namna inavyotumia ardhi katika kufanikisha kilimo bora.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe kutokea WFP, Neema Shosho alisema WFP inatekeleza mradi wa Boresha Lishe chini ya udhamini wa EU, wenye thamani ya Euro milioni 24.5 kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa lishe na kilimo bora kwenye mikoa ya Singida na Dodoma.
Alisema, mradi huo wa miaka mitano, huu ukiwa ni mwaka wake wa pili, umeshawabadilisha mtazamo wananchi wa mikoa hiyo na kupenda kujihusisha na kulima chakula chenye lishe bora.
Alisema, mradi huo unafanya kazi kwa ukaribu zaidi na wananchi hasa watendaji wa ngazi za vijiji kwa kuwapatia elimu bora ya kufuga, kulima pamoja na kusimamia utekelezwaji wa mradi huo. Alisema, mradi huo umesaidia pia kuongeza kipato cha wananchi kwa kuwa licha ya kulima na kufuga kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani pia wanalima na kufuga kibiashara
