Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kushirikiana na wadau kukuza Kiswahili



Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakua na kuendelezwa ili kuiwezesha kuelezea masuala ya nyanja nyingine badala ya lugha yenyewe.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mshiriki wa Tataki, Dk Mussa Hans wakati akifungua warsha ya utengenezaji wa kamusi ya Kiswahili ya Astronomia iliyofanyika katika Kituo cha Mkoa cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania cha Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kushirikiana na wadau mbalimbali katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kutokana na kupanuka kwa lugha hiyo kimawanda ambako kunaifanya kuhitaji msamiati maalumu katika uwanja mahususi.

Kukamilika kwa kazi hii ya utengenezaji wa kamusi kutasaidia kutumika kwa lugha hii kuwafikia Watanzania wengi na pia kuwapa heshima kubwa; alisema Dk Hans. Aliwataka wataalamu hao kutanguliza mbele maslahi ya umma, uzalendo na moyo wa kujitolea kwa kuwa kazi hiyo ina changamoto mbalimbali hivyo kusaidia ukamilishaji wa kazi hiyo katika ubora.

Aidha aliwaasa washiriki kukumbuka historia ya nchi na waliotangulia katika kufanya kazi kama hizo ili kupata kamusi itakayofuata kanuni na muundo wa lugha ya Kiswahili badala ya kuja na maneno mapya kwa jamii ambayo yatafanya Kiswahili kuonekana kama lugha ngumu. Dk Noorali Jiwaji wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alisema kumekuwa na tatizo katika vitabu na vitini vya kufundishia hususani lugha ya Kiswahili katika ngazi ya shule ya msingi.

Kamusi ya Astronomia ya Kiswahili itakapomilika, itasaidia kupata sehemu ya marejeleo kwa walimu ili kurahisisha ufundishaji wa masuala ya masuala ya elimu ya anga; alisema Dk Jiwaji. Kwa upande wake, mwanafunzi Mwasiti Shaban anayesomea Stashahada ya Uhandisi wa Majengo katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) alisema kwa kuwa elimu ya astronomia nchini ipo chini kuna umuhimu wa Watanzania kuhakikisha fani hiyo inakua na kufahamika kuanzia ngazi ya chini.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali katika fani za sayansi katika ngazi za elimu kutoka shule za msingi hadi vyuo vikuu ikiwemo Fizikia, Hisabati, Kemia bila kusahau wataalamu wa lugha ya Kiswahili
Mpya zaidi Nzee zaidi