Na.Thabit Madai, Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaendelea kutekeleza mpango madhubiti katika kuhakikisha wanasimamia ipasavyo sheria na kanuni zilizopo nchini ili kulinda zao la karafuu isiuzwe kimagendo hali inakayopelekea kukosesha Serikali kukusanya mapato kikamilifu yatokanayo na zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar Balozi Amina Salum Ali Wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika la Biashara la Taifa, Zanzibar (ZSTC) ambapo kilele cha maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kesho katika hotel verde iliyopo mtoni Marine mjini magharib Unguja na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Ali mohammed Shein.
Balozi Amina Alisema hatua hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti usafirishaji wa karafuu kwa njia za magendo nje ya nchi ambapo hali hiyo zanzibar itapoteza sifa ya kuwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo.
“tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano na serikali kuwabaini hawa wagodo wadogo wanaondelea kuuza karafuu kwa njia za magendo” alisema Balozi Amina.
Aidha Balozi Amina Alisema serikali inaendelea kusimamia kanuni na sheria hizo ili zao karafuu liendelee kuwa kuwa tegemezi katika kukuza uchumi wa zanzibar.
Akizungumzia mafanikio ya shirika la biashara zanzibar alisema shirika hilo limepata mafanikio makubwa yakiwemo kutoa mikopo kwa wenye mashamba ya karafuu na kuongeza bei ya zao hilo kwa wakulima kwa lengo la kuwasaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi.
Aidha amefahamisha kuwa Shirika hilo limeimarika kwani kwa sasa na limeweza kulipa fidia kwa wale wanaopata ajali ya kuanguka mkarafuu pamoja na kutoa vifaa kwa ajili ya wakulima wa zao hilo.
Balozi Amina ameeleza kuwa katika azma ya kuliimarisha ili kurudia hadhi yake Shirika limeweza kufunga mkataba na kiwanda cha makonyo kutoka China na kufufua mashamba ya viungo asilia ili kuweza kupata pato zaidi na kuimarika kiuchumi.
Amefahamisha kuwa kufufuliwa kwa shirika kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na biashara pamoja na vijana wengi watapa ajira na kuendeleza pato la taifa.
