Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ametembelea Kituo cha Umahiri cha Bariadi ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kumhaidi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kuwa, Wizara ya Madini itaangalia namna ya kuusaidia mkoa huo katika uendelezaji wa madini ya Nikel na chumvi yanayopatikana mkoani humo.
Pia, Waziri Kairuki ametoa pongezi kwa Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo hicho kwa kazi iliyofanyika na kumtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa kukamilisha ujenzi na ubora wake.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuridhia kuondoa tozo 9 kati ya 16 zilizokuwa zikitozwa na Taasisi mbalimbali za serikali katika Sekta ya Madini.
Amesema uwepo wa kituo hicho mkoani humo, utawezesha wachimbaji wadogo wa madini kuchimba kwa tija.
Pia, ametoa rai kwa wananchi walio tayari kuwekeza katika Sekta ya Madini kuwekeza mkoani humo pamoja na maeneo mengine nchini.
Vilevile, amewataka wale wenye leseni za madini kutoshikilia leseni hizo bila kuziendeleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka, ameishukuru Wizara kwa kuuchagua mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa ambayo vituo hivyo vya umahiri vinajengwa.
Amesema kuwa, uwepo wa kituo hicho utawezesha wachimbaji kupata mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija ikiwemo kupata mahali sahihi ambapo shughuli za uendelezaji Sekta ya Madini utafanyika.
Aidha, ameleeza pia, kituo hicho kitatumika kama sehemu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi ikiwemo taarifa kuhusu bei elekezi ambazo wizara kupitia Tume ya Madini imekua ikitoa kila mwezi.
Vituo vya Umahiri vinajengwa na mkandarasi kampuni ya SUMAJKT maeneo mbalimbali nchini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia.
