Na Enock Magali,Dodoma
Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dodoma kimeazimia kuiomba Serikali kuongezea fedha kwa Wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) ambayo hadi sasa wamekwisha pewa asilimia 46 pekee ya bajeti yao hadi hivi sasa.
Aidha mtandao wa Barabara zinazosimamiwa na TARURA ni zaidi ya km elfu sita ambapo katika bajeti wamepewa kiasi cha Shilingi Bilioni 14.7.
Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara mkoani Dodoma,Mkuu wa Mkoa huo Dk.Binilith Mahenge amesema barabara ndio Injini na kiungo kikubwa cha Uchumi hivyo kuiomba Serikali kuwezesha wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara vijijini na mijini (TARURA).
“Wenzetu wa TARURA mtandao wao ni km elfu sita na zaidi,lakini ndio Bilion 14.7 kwaiyo bado mahitaji ya fedha tunahitaji ziongezeke zaidi na ndio maana kwenye kikao cha Bodi ya barabara kimeazimia kuiomba Serikali ilendelee kutoa fedha zaidi hasa kwenye mfuko wa barabara TANROAD ili waweze kujenga barabara za mkoa ili ziweze kupitika vizuri lakini pia tumeona ni vizuri kuiomba Serikali ituongezee fedha kwa wakala”Alisema
Aidha pia Dk.Mahenge ameagiza kushirikishwa kwa viongozi wa ngazi za vijiji na kata ili kukabiliana na wafugaji ambao wamekuwa wakipitisha mifugo na kuharibu barabara.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA jiji la Dodoma Mhandisi Ephrahim Mkinga amesema,kuwa suala la fedha ni jambo la msingi lililopo kwa TARURA na kuwa uwiano wa kibajeti kati yao na TANROAD hauko sawa kutokana na kuwa wao wana mtandao mkubwa wa barabara.
“TANROAD wana km 1600 lakini TARURA tuna km 6685 lakini pia tunahudumia jamii kubwa sana ambayo tunakuja kuhudumia barabara za TANROAD ,kwaiyo kama ambavyo kikao kimeona TARURA iongezewe bajeti iko sawa”Alisema.
Akiwasilisha Mpango wa utekelezaji wa miradi ya barabara zilizochini ya TANROADS katika kikao hicho Meneja wa Wakala Mkoa wa Dodoma (TANROAD) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Leonard Chimagu amesema kuwa TANROAD imepata hasara ya Shilingi Milioni 371.7 katika mwaka wa fedha 2018/2019 kutokana na uharibifu wa miundombinu ya barabara .
Chimagu amesema hasara hiyo inatokana na wizi wa alama za barabarani ambao umesababisha hasara ya Shilingi Milioni 10.5 na wakati uharibifu wa mabega ya barabara unaotokana na uegeshaji holela uliosababisha hasara ya Shilingi Milioni 361.2 na hadi sasa kuna maeneo yaliyoharibika hayajatengenezwa.
Lakini pia ametaja changamoto wanazo kabiliana nazo kuwa uegeshaji holela wa magari makubwa kandokando ya barabara unaosababisha kukatika kwa kingo za barabara na kuisababishia wakala huo hasara kubwa.
