Mbunge Mary Nagu awataka wananchi waungane pamoja na serikali


Na. John Walter, Hanang

Mbunge wa jimbo la Hanang mkoani Manyara  Mary Nagu (CCM) amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuungana  na Serikali katika kuleta maendeleo katika  maeneo yao na Taifa kwa ujumla  na si kutegemea serikali Pekee na wahisani.

Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki hii wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo  katika Mkutano wa hadhara kwa Kata nne za Tarafa ya Balang'dalalu ambapo amesema kuwa  ili kuleta maendeleo kwa haraka wananchi wanapaswa kuungana katika kuchangia maendeleo hayo.

Amesema kipindi chake cha uongozi kama Mbunge anajivunia kutekeleza ahadi alizoahidi kwa wananchi wake ikiwemo Miundo mbinu ya barabara ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa katika jimbo hilo  hivyo wananchi nao wanapaswa kuendeleza pale alipoishia.

"Awali jimbo hili lilikuwa na changamoto ya miundombinu  ya barabara, maji, madarasa lakini katika kipindi changu cha ubunge nimefanikiwa kutengeneza bara bara katika Tarafa za Simbay na Balang’dalalu na Kata zote za jimbo hili  huku zingine zikiendelea kukarabatiwa",

Aidha  Mbunge huyo amewaleza wakazi wa Jimbo la Hanang kuwa kwa sasa Serikali kupitia wakala wa barabara vijijini (TARURA) wataendelea kujenga barabara katika vijiji vyote ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na urahisi wa kwenda kupata huduma za  afya.

Kuhusu suala la nishati ya Umeme,Nagu amesema Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA)  imedhamiria kufikisha umeme  katika Vijiji vyote Nchini  ifikapo 2020 hivyo wahakikishe hawapitwi na fursa hiyo.

Amefafanua kuwa  ili kuhakikisha vijiji  vinapata maji,Serikali imeunda  mfuko wa  maji  Vijijini ambao unashughulikia changamoto hiyo, hivyo waendelee kuvumilia kwani hakuna nyumba inayojengwa siku moja.

“Pamoja na hayo, Rais wetu amerudisha nidhamu ya kazi serikalini kwani kwa sasa nchi inakusanya kodi kwa uhakika, huduma za afya zimeimarishwa, miundombinu ya barabara imeimarishwa pia, maji, umeme na elimu bure inatolewa,” alisema Nagu.

Wakati mbunge akiyazungumza hayo,Wananchi wamekuja juu na kueleza kuwa tatizo la maji limekuwa likiwakabili kwa muda mrefu huku viongozi wakiwa kimya na kumuomba  mbunge wao  awatatulie changamoto hiyo  mapema na sio kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items