Wahukumiwa miaka 40 jela, Kisa?


Na. Raheli Nyabali, Tabora

Watu wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka 40 baada ya kuwakuta na hatia ya kutenda  makosa matatu  kinyume  cha  sheria ikiwemo Kesi ya uhujumu  uchumi iliyokuwa  inawakabili katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora.

Akisoma hukumu hiyo hakimu  mkazi Mkoa wa Tabora, Jocktan Rushwela  amesema  mahakama  baada ya kupitia maelezo ya mashtaka yaliyowasilishwa na Wakili Upande wa  Jamhuri  Mercy Ngowi,iliamua  kujiridhisha  kwa  kupitia maelezo  ya  ushahidi wa  pande  zote  mbili na  kubaini  kuwa  watuhumiwa Ibrahim Mbaruku  na  Yassin Mohammed walitenda makosa  hayo  kinyume  cha  sheria ya  uhifadhi  na  wanyama  pori  namba tano ya mwaka 2009 wakiwa  ndani  ya  hifadhi  ya  pori la Ugalla.

Kwa  makosa matatu  yaliyowatia  hatiani  katika shitaka  hilo la uhujumu uchumi namba 4 la  mwaka  2017,kosa  la  kwanza kuingia  ndani ya  hifadhi ya msitu  wa  pori la Ugalla bila  kibali halali  adhabu  iliyotolewa ni  kutumikia  kifungo cha mwaka mmoja jela  au  kulipa  faini  ya  shilingi laki moja.

Katika Kosa la pili ambalo ni kukutwa na silaha  aina ya Gobore  ndani ya hifadhi ya Ugala  iliyopo  wilayani  Kaliua  adhabu  iliyotolewa  ni  kutumikia  kifungo  cha  miaka  ishirini  Jela.

Aidha kosa la tatu ni kukutwa na nyara za Serikali  ikiwemo mzoga wa mtoto wa Simba  ndani  ya  Pori  hilo  la Ugala washtakiwa wamehukumiwa  kutumikia  kifungo  cha  miaka  ishirini  kwa kila  mmoja  na  kufanya  jumla  ya  adhabu  ya kifungo  cha  miaka  41  kwa  kila  mshtakiwa.

Hakimu  mkazi Mkoa wa Tabora, Jocktan Rushwela akafafanua mbele ya washitakiwa hao wawili kwa adhabu ya kosa la pili na la tatu  wataitumikia  kwa  pamoja  kwa  kifungo  cha  miaka  ishirini huku adhabu ya mwaka mmoja kwa  kosa la kwanza ikisalia pale pale.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items