TAKUKURU yafuatilia miradi ya Sh. Bilioni 39.8


Katika robo ya kwanza ya mwaka 2019, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma iliendelea na majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.

TAKUKURU imefuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni thelathini na tisa na milioni mia nane (39,800,000/=) ili kujiridhisha iwapo fedha zinatumika vizuri kwa wakati na iwapo miradi inatekelezwa kwa ubora na thamani halisi ya fedha inapatikana. Miradi iliyofuatiliwa ni katika sekta za maji, ujenzi, elimu na afya. 

Katika miradi iliyofuatiliwa, fedha Sh. milioni mia tisa (900,000,000/=) inachunguzwa baada ya viashiria vya jinai kuonekana. TAKUKURU pia imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. milioni mia moja hamsini na mbili na laki tatu (152,300,000/=) ambazo zingelipwa kwa wakandarasi ambao ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maji umebaini hawakutimiza majukumu yao ipasavyo. Pia tumebaini udanganyifu katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mima wilayani Mpwapwa hivyo tunamtaka Mkurugenzi wa kampuni ya Global Space East Africa Limited ya DSM Bw. Gaston Meltus Francis ambaye kampuni yake ilipewa kazi hiyo kuripoti mara moja kwenye ofisi zetu za wilaya ya Mpwapwa.

Aidha, TAKUKURU imefanya uchambuzi wa mifumo mbalimbali ili kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna bora ya kuondokana nayo kwa lengo la kudhibiti vitendo vya rushwa. Jumla ya mifumo nane (8) ilichambuliwa katika sekta za maji, elimu, afya na ukusanyaji wa mapato kwa mtandao. Katika uchambuzi mmojawapo imebainika kwamba ukusanyaji wa mapato kwa kutumia POS una mianya kadhaa ya rushwa na upotevu wa mapato hivyo ushauri wa kuziba mianya hiyo umetolewa.

TAKUKURU iliendelea na jukumu la kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali, lengo likiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kivitendo katika mapambano dhidi ya rushwa. Uelimishaji ulifanywa kwa kuendesha semina 31 kwa makundi mbalimbali na mikutano ya hadhara 47 kwa wananchi. Pia tumeendesha vipindi vya redio ambapo mkazo mkubwa uliwekwa kwenye elimu dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na kudhibiti rushwa ya ngono.

Aidha, katika kuandaa Taifa la vijana wanaoichukia rushwa, vilabu 105 vya wapinga rushwa katika shule za msingi na sekondari vilifunguliwa na vilabu 41 vya zamani vilitembelewa kwa lengo la kuviimarisha.

Katika kipindi husika, TAKUKURU ilipokea jumla ya taarifa tisini na sita (96) za rushwa na makosa yahusianayo ambapo sekta zifuatazo ziliongoza kwa tuhuma: Serikali za mitaa (25%); Ardhi (17%); Elimu (16%); Afya (8%); Maji, Ujenzi na Mahakama (kila moja asilimia 7); na Polisi (6%). Taarifa hizo zilifanyiwa kazi kwa njia mbalimbali na majalada nane (8) ya uchunguzi yalikamilika ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.5 ya majalada yaliyokamilika kwa kipindi hicho mwaka 2018. Aidha tumefungua kesi mpya tano (5) na kesi nne (4) zilitolewa maamuzi na Mahakama ambapo Jamhuri imeshinda zote kwa washtakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali.

Kwa robo ya Aprili hadi Juni, 2019, pamoja na majukumu mengine TAKUKURU inakusudia kuongeza juhudi katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati mkoani Dodoma ikiwemo ya ujenzi wa barabara; kuchambua mifumo ya ukusanyaji wa kodi na mapato ya serikali; na kuendelea kuelimisha umma madhara ya rushwa katika uchaguzi.

TAKUKURU inawasihi wajumbe wa Kamati za Ujenzi na Manunuzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kuzingatia taratibu za matumizi ya fedha za serikali na kuwaasa wasikubali kurubuniwa na viongozi wasio waadilifu kwani wao ndio watakaowajibika. Pia tunawataka watendaji kutupatia nyaraka tunazohitaji kisheria kwa wakati ili tutekeleze majukumu yetu na kuwaasa wale wanaojaribu kutukwamisha kwamba kitendo hicho ni kosa la jinai na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.

Tunawashukuru wananchi kwa kutupa ushirikiano na tunawaomba waendelee kuwa na uthubutu wa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wakati. TAKUKURU itafanyia kazi taarifa zote hata kama wahusika wapo maeneo ya mbali ya vijijini.

Imetolewa na: 
Sosthenes Kibwengo
Mkuu wa TAKUKURU (M) Dodoma 

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items