Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika huenda akajiuzulu wiki hii baada ya maandamano makubwa na shinikizo linalotolewa na jeshi la kumtaka kuachia ngazi baada ya miaka 20 ya utawala wake.
Kulingana na kituo binafsi cha televisheni nchini humo cha Ennahar, Bouteflika anajiandaa kujiuzulu kulingana na kifungu cha 102 cha katiba.
Ripoti hizi zinatolewa masaa kadhaa baada ya rais Bouteflika kutaja baraza la mawaziri ya serikali ya mpito.
Hakukua na ripoti kama hiyo iliyotolewa vyombo vya habari vya serikali, na ofisi ya rais haikupatikana mara moja kujibu taarifa hiyo.
Chanzo kimoja cha kisiasa kimesema hatua hii inaashiria Bouteflika huenda akajiuzulu kwa kuwa rais wa mpito hatakuwa na mamlaka ya kuchagua baraza.
Waziri mkuu anayekabiliwa na changamoto Nouriddine Bedoui ataliongoza baraza hilo, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali, APS, lililotaja mawaziri hao 27 wa baraza la mpito.
