Marekani yawaondoa wafanyakazi wake Iraq


Wizara ya maswala ya kigeni nchini Marekani imeagiza kuondoka kwa wafanyakazi 'wasiofanya kazi za dharura' nchini Iraq kufuatia hali ya wasiwasi kati ya Marekani na Iran.

Wafanyakazi katika ubalozi mjini Baghdad na wale wa ubalozi wa Irbil wametakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo katika uchukuzi wa kibiashara, Ujerumani wakati huohuo imesitisha mafunzo ya wanajeshi wake nchini Iraq.

Jeshi la Marekani lilisema siku ya Jumanne kwamba kiwango cha vitisho hivyo mashariki ya kati vilitolewa kutokana na ujasusi kuhusu vikosi vinavyoungwa mkono na Iran katika eneo hilo.

Ni kinyume na matamshi ya Jenerali mmoja wa Uingereza aliyesema kuwa hakuna vitisho vyovyote vilivyoongezeka.

Chris Ghika ambaye ni Naibu kamanda wa muungano wa majeshi dhidi ya kundi la wapiganaji wa Islamic State, aliwaambia maripota kwamba hatua zilizochukuliwa kuwalinda wanajeshi wa Marekani na washirika wao kutokana na vikosi vinavyoungwa mkono na Iran nchini Iraq na Syria zinatosha.