Kinyang'anyiro kiti cha uwaziri mkuu Uingereza chapamba moto

Wagombea waliomo katika mbio za kuwania kiti cha waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wanatarajiwa kupungua leo wakati wabunge wa chama cha Conservative watakapopiga kura kumuondoa angalau mgombea mmoja kati ya wagombea 10 katika kura ya kwanza, licha ya kuwa Boris Johnson anaongoza kundi la wagombea.

Uingereza inaweza kuwa inaelekea katika mzozo wa kikatiba kuhusiana na Brexit kwa kuwa wagombea wengi wanaowania kumrithi May wanajitayarisha kuiondoa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya Oktoba 31 bila ya makubaliano lakini bunge limeonesha kwamba litajaribu kuzuwia hatua kama hiyo.

Mmoja kati ya wagombea hao, waziri wa mambo ya ndani Sajid Javid amesema Uingereza inapaswa kuwa tayari kujitoa bila makubaliano ifikapo Oktoba 31.

Amesema umuhimu wake mkubwa anauweka katika kufanikisha makubaliano ya Brexit lakini serikali inapaswa kuchukua hatua za ziada kujitayarisha kujitoa bila makubaliano.
Mpya zaidi Nzee zaidi