Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka watu wenye ualbino kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa wanavyopatiwa kwaajili ya kukabiliana na changamoto ya saratani ya ngozi.
Alisema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Dk Kebwe Stephen Kebwe kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa wa ualbino iliyofanyika juzi kitaifa mkoani Morogoro. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Stella Ikupa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni afya bora ,ustwai kwa wote : Tanzania bila saratani kwa wenye Ualbino inawezekana. Makamu wa Rais alisema baadhi yao wamejenga tabia ya mazoea ya kuiga mambo ambayo yanachangia kwa kiwango kikubwa cha upatikanaji wa saratani ya ngozi.
Mathalani kundi la vijana wamekua na tabia ya kuvaa nguo fupi na zenye kuonesha sehemu kubwa ya mwili wao jambo hili linahatarisha kupata saratani ya ngozi" kupitia hadhara hii kila mmoja wetu awe balozi na aendelee kutoa elimu hii katika jamii,"alisema Makamu wa Rais.
Alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa watu wenye ualbino na kuwa katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea kwa kundi hilo , tayari serikali kwa kushirikiana na wadau imeanza kutoa muongozo wa utoaji wa huduma za elimu kwa wanafunzi wenye ualbino unaoelekeza namna bora ya kuwahudumia.
Makamu wa Rais pia alisema kuwa licha ya suala la takwimu za watu wenye ualbino limekuwa bado ni changamoto hapa nchini, ila rejista imeshaanza kuandaliwa ili kuhakikisha uwepo wa takwimu za watu wenye ulemavu ikiwepo kundi hilo.
Alisema hatua hiyo ni kama ilivyo kwa mujibu wa matakwa ya sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2019 sehemu ya 6 kifungu cha 23(1-3). Naibu Waziri alitoa wito kwa wazazi wote wenye watoto wenye ualbino na kulelewa katika vituo mbalimbali kwa kuhofia usalama, kwenda kuwachukua kwa vile kwa sasa hali ni shwari.
Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ualbino Tanzania ( TAS), Names Temba akisoma risala ya maadhimisho hayo alibainisha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo kwa wanafunzi wenye ualibino na uoni hafifu. Temba alisema kuwa, licha ya changamoto kadhaa zinazowakabili wanafunzi hao wanahitaji kuwa na vitabu maalumu vya maandishi yaliyokuzwa kwa ajili yao
