Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana hotuba ya bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020 jana katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020, hatapelekwa katika kamati ya Bunge ya maadili.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Spika wa bunge, Dk Tulia Ackson ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni kama alivyopendekeza kaimu mnadhimu wa kambi hiyo, Joseph Selasini kwa maelezo kuwa hata mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya aliwahi kurusha vitabu bungeni na kuvichana lakini hakupelekwa katika kamati hiyo.
Hapo jana wabunge wa CHADEMA, Esther Matiko, John Heche na Dkt. Emmaculate Sware walitolewa Bungeni wakipinga Dkt. Tulia kumtaka Augustine Vuma(CCM) kuomba radhi kwa alichokizungumza wakati akichana kitabu cha hotuba ya Upinzani na si kitendo chake cha kuchana kitabu.
