Na Ahmad Mmow, Kilwa.
Halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoani Lindi imekumbushwa na kuombwa itekeleze kwa vitendo agizo la naibu waziri wa wizara ya mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega.
Akizungumza na Muungwana Blog, mwenyekiti wa vikundi nane vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari na pwani(BMU) vilivyopo wilayani Kilwa, Maulid Mbulula alisema halmashauri ya wilaya ya Kilwa hainabudi kuvipa uwezo na haki ya kukusanya ushuru wa mazao ya uvuvi na bahari vikundi hivyo kama alivyo agiza waziri Ulega.
Alisema, Ulega wakati anakabidhi boti iliyotolewa na shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira(WWF) kwa halmashauri hiyo aliitaka ivipe uwezo na haki ya kukusanya ushuru ili malipo ambayo yangetolewa kwa kampuni au watu binafsi kwa kazi hiyo yapewe vikundi hivyo ili vimudu kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Mbulula alisema agizo la waziri Ulega ambalo halijafanyiwa kazi lilikuwa ni jema kwa uimara na uhai wa vikundi hivyo ambavyo vinashirikiana na serikali kupambana na uvuvi haramu na uhalifu mwingine wa baharini na pwani ya bahari ya Hindi katika wilaya ya Kilwa.
'' Tunaishukuru WWF kwakutoa boti kwa ajili ya doria na kuvipatia mafunzo vikundi hivi. Hata hivyo baadhi ya vikundi vinahali mbaya kiuchumi, vitashindwa kumudu kutimiza wajibu wake. Halmashauri itekeleze agizo lile na itoe mafunzo, kwasababu vikundi vingi vinafanya kazi bila weledi,'' alisisitiza Mbulula.
Mbali na hayo, mwenyekiti huyo alisema vitendo vya uhalifu baharini na pwani, hasa uvuvi haramu vimepungua. Hata hivyo bado kunahaja ya kuongeza juhudi katika kufanya doria. Kwani uvuvi haramu na zana haramu bado zipo.
Juhudi za kumpata mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa zinaendelea. Kwani hadi habari hii inaandikwa alikuwa hapatikani hewani.
Nahata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu haikurudi taarifa ya ujumbe huo kumfikia. Lengo lilikuwa nikutaka kujua kutoka kwa mkurugenzi mtendaji huyo wa halmashauri ya wilaya(DED), Renatus Mchau anazungumziaje madai hayo na kama nikweli naibu waziri huyo alitoa agizo hilo.
