Makamu wa Rais afungua Jukwaa la Sita la Maendeleo Endelevu


Na. Enock Magali, Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31 amefungua Jukwaa la Sita la Maendeleo endelevu juu ya usimamizi madhubuti wa misitu kwa ajili ya upatikanaji wa Rasilimali maji endelevu Nchini.

Jukwaa hilo lililoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI,limefunguliwa Jijini Dodoma na kuwakutanisha wawakilishi mbalimbali kutoka Serikalini ,Sekta binafsi, Asasi za kiraia,Taasisi za kielimu na kiutafiti pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza katika Jukwaa hilo Makamu wa Rais Mama Samia,amewasihi wananchi kutunza mazingira kwani suala la upatikanaji wa maji nchini bado si la kuridhisha kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kufanywa katika maeneo mbalimbali nchini.

"Ni kweli kuwa kwa sasa vyanzo vingi vya maji vimekauka,kule ambako zamani watu walikuwa wakienda na kuchota maji,tumekata miti na kuchafua vyanzo vya maji na tumekausha pia,kwa hiyo upatikanaji wa maji umekuwa mgumu sana,Serikali inatumia rasilimali nyingi sana kuvuta maji kutoka kwenye vyanzo na kupeleka kwa wananchi,"Alisema.

Aidha Mama Samia ameitaka Taasisi ya UONGOZI kuweka ufatiliaji wa yale yatakayo kubaliwa katika kongamano hilo,ili kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji mzuri wa maadhimio hayo.

"Makongamano haya tumekwisha fanya mengi mno,lakini tukitoka hapa hakuna tena ufatiliaji,ni imani yangu kuwa Taasisi ya UONGOZI baada ya Kongamano hili watafuatilia ili kuhakikisha kwamba yale yote yaliyo kubaliwa hapa yanatekelezwa vizuri."Aliongeza.

Akizungumza katika Kongamano hilo,Waziri wa nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Mh.George Simbachawene,yeye amekiri kutoridhika na hayuko tayari kuona rasilimali nyingi zinazotolewa haziendi moja kwa moja katika mazingira yanayo haribika.

"Siridhiki.sifurahishwi na sipo tayari kuona rasilimali nyingi haziendi moja kwa moja kwenye mazingira halisi yanayo haribika,Sisi tunaokaa kwenye vyumba hivi vya mikutano hatuishi moja kwa moja kwenye vyanzo vya maji vinavyoharibika,kila siku tuko kwenye vyumba vya mikutano lakini kule kila siku misitu inaharibiwa, "Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amesema awamu zote za uongozi zilizopita zimefanya mambo makubwa lakini kumekuwa hakuna utekelezaji wa maazimio yanayotolewa hivyo kushauri kuzingatiwa kwa maadhimio yote yatakayo adhimiwa.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa wa Taasisi ya UONGOZI, Prof. Joseph Semboja,amesema kuwa Jukwaa hilo la Maendeleo endelevu lilianzishwa mwaka 2012 kwa lengo la kuwakutanisha viongozi na wadau mbalimbali kujadili na kuhamasisha maendeleo endelevu ,maendeleo jumuishi yanayo zingatia utunzaji wa mazingira na matumizi madhubuti ya rasilimali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vya baadaye.
Mpya zaidi Nzee zaidi