Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania inajivunia kufanya kazi kwa karibu na Nchi ya Rwanda kutokana na ukarimu mkubwa uliojengeka kwa muda sasa kwa Wananchi wa Nchi mbili hizo.
Makamu wa Rais amesema hayoalipokutana na Balozi wa Rwanda Nchini Tanzania, Eugene Kayihura wakati Balozi Kayihura alipofika Ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu Jijini Dar es salaam leo kwa ajili ya kumuaga Makamu wa Rais Baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa Nchini.
Makamu wa Rais amemuhakikishia Balozi Kayihura kwamba Tanzania itaendelea kudumisha Uhusiano wa Nchi mbili hizi uliodumu kwa muda mrefu sasa katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kijamii hasa katika kuangalia fursa za kiuchumi pamoja na kuwa na uhusiano mzuri wa huduma ya Fedha kati ya Rwanda na Tanzania.
Samia amesema muda umefika sasa kushirikiana pamoja kwa ajili ya kujenga Uchumi wa Mataifa haya, ambapo pia amempongeza Balozi Eugene Kayihura kwa Ushirikiano Mkubwa alioutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kipindi chake chote cha kazi hapa Nchini na kumtakia kila la Heri kokote aendako katika kituo chake kipya cha kazi.
